Wilshere aambiwa aondoke

LONDON, ENGLAND
JACK Wilshere amefichua kuwa ameambiwa na Kocha Arsene Wenger aondoke Arsenal.
Wilshere aliripotiwa kuwa kwenye mazungumzo ya mkataba mpya wa kuendelea kubaki Emirates, lakini amedai Kocha Wenger amemshauri tu akatafute timu nyingine ya kuichezea.
“Aliniambia ‘nataka kuwa mkweli kwako kwa wakati huu hatuwezi kukupatia mkataba mpya. Hivyo, kama watakupigia simu huko kwingineno, unaweza kwenda,’" alisema Wilshere akifichua kile alichoelezwa na Wenger
“Nilikuwa gym kwa wakati huo, nikaduwaa sikutoka chumbani. Kilikuwa kitu cha kushangaza kidogo, labda kuna waliokuwa wakilifahamu hilo, nilichokuwa nakitaka ni kupata uhakika tu kuwa klabu inanichukuliaje.
“Nilisema napigania namba yangu. Na siku zote nilikuwa na uhakika nitarudi na kupata namba kwenye kiungo pindi nitapokuwa fiti bila ya kusumbuliwa na majeraha. Nilithibitisha hilo na nilirejea kwenye timu."
Wilshere alisema hilo lilitokea kwenye dirisha lililopita ambapo Kocha Wenger aliamua tu kuwa mkweli kwa kumwaambia vitu bayana.
Kiwango cha Wilshere kwa siku za karibuni kimerejea kwenye ubora wake na kufanikiwa kupata namba katika Timu ya Taifa ya England, ambayo ipo kwenye maandalizi kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika baadaye mwaka huu huko Russia.