Wasipofanya ‘uchawi’ huu hawachezi

LONDON, ENGLAND. KATIKA soka, kuna baadhi ya wachezaji huwa na mambo ya kushangaza sana, baadhi hufanya mambo yao kabla ya mechi na kuna wale ambao hufanya yao baada ya mchezo kufanyika.

Baadhi ya wachezaji wamekuwa na kawaida ya kusikiliza wimbo fulani, wengine wamekuwa wakifanya kitu kuhusu jezi zao, nywele zao na wengine kusali kabisa.

Lakini, kitu cha kujiuliza jambo hilo lina umuhimu gani hata wakalifanya mara kwa mara kabla au baada ya mechi wanazocheza? Hawa hapa, wanasoka watano ambao wamejenga tabia ya kufanya mambo yao katika kila mechi wanazopaswa kuingia uwanjani na kucheza. Ndio uchawi wao? Wanajua wenyewe.

5. Neymar – kuzungumza na baba yake

Supastaa wa Kibrazili, Neymar, hii ya kwake ndio kali zaidi. Straika huyo wa PSG haingii uwanjani kwenye mechi yoyote kama hajazungumza na baba yake kwanza.

Atafanya hivyo iwe kwa mazungumzo ya ana kwa ana kama atakuwapo uwanjani hapo, au kwa kumpigia simu kama atakuwa mbali.

Kusikia sauti ya baba yake ndicho kitu kinachompa Neymar nguvu na maarifa ya kwenda kufanya vizuri ndani ya uwanja. Baba yake ndiye mtu ambaye amekuwa naye bega kwa bega katika maisha yake yote ya soka.

4. Javier Hernandez – kupiga magoti na kusali

Mshambuliaji matata kabisa wa Mexico, Javier Hernandez, amekuwa akipiga magoti na kusali kabla ya kila mechi anayopaswa kucheza. Amekuwa akifahamika kwa hilo, kwamba kabla ya mechi kuanza, lazima kwanza afanya jambo lake hilo. Ndiyo staili yake ya kuomba dua na kusali. Staa huyo anayefahamika kwa jina la Chicharito ni mkristo.

3. Luis Suarez – kubusu kifunDo cha mkono na vidole

Straika wa Barcelona na timu ya taifa ya Uruguay, Luis Suarez, amekuwa na kawaida ya kubusu pete yake ya ndoa na kisha kwenye kifundo chake cha mkono kila anapofunga bao iwe kwenye klabu au timu ya taifa. Kwenye kifundo cha mkono, kuna tattoo ya majina ya watoto wake. Staa huyo wa zamani wa Liverpool amekuwa akivibusu pia vidole vyake kila anapofunga bao.

2. Cristiano Ronaldo – kukata nywele

Supastaa wa Ureno na klabu ya Juventus, Cristiano Ronaldo, amekuwa na kawaida ya kukata nywele kabla ya kila mechi anayocheza.

Ronaldo amekuwa akifanya hivyo hata kama mechi moja na nyingine zimetofautiana kwa siku tatu tu, lakini lazima akate nywele zake kabla hajacheza mechi nyingine.

1.Mesut Ozil – kusoma Quran

Staa wa Arsenal, Mesut Ozil, huwa anasoma Quran kabla ya kila mechi anayocheza.

Marafiki zake wanalitambua hilo kwamba ni muhimu kwake kufanya hivyo kabla ya mechi, hivyo hakuna anayekwenda kumsumbua huwa wanamwacha afanye mawasiliano na Mungu wake kuomba dua za kushinda.