Wamoroccoo wambakiza Msuva Dar

Muktasari:

Msuva amelazimika kubaki nchini, ili kushughulikia Viza ya kwenda Morocco kujiunga na klabu ya Difaa El Jadida.

KIKOSI cha timu ya taifa, Taifa Stars imeshatua mjini Kigali kwa ajili ya mechi yao ya kesho na wenyeji wao Rwanda, lakini huku nyuma winga tegemeo wa timu hiyo, Simon msuva amesalia jijini Dar es Salaam.
Msuva amelazimika kubaki nchini, ili kushughulikia Viza ya kwenda Morocco kujiunga na klabu ya Difaa El Jadida.
Msuva aliliambia Mwanaspoti, yupo nchini kwa ajili ya kukamilisha visa ili aweze kwenda Morocco kujiunga na timu hiyo ambayo tayari imemalizana na Yanga.
“Sijaenda Rwanda, nafuatilia visa, ipo katika hatua ya mwisho. Viza ikitoka ndio watanitumia tiketi ili niende moja kwa moja kule," alisema.
Msuva alisema mpaka sasa hajasaini kwa Wamorocco hao, lakini walizungumza awali na kukubaliana na kila kitu, hivyo kinachompeleka nchini humo ni kumwaga wino na kisha kuanza kukitumikia kikosi hicho cha Ligi Kuu na kitakachoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Msuva ni miongoni mwa nyota walioibeba Stars ya Kocha Salum Mayanga kilichotwaa nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Cosafa akifunga mabao mawili, lakini atakosekana katika mchezo wa kesho kuwania fainali za Chan 2018.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa CCM Kirumba, Mwanza Stars ililazimisha sare ya 1-1 mbele ya Amavubi waliotangulia kupata bao kabla ya Himid Mao kusawazisha kwa mkwaju wa penalti. Mshindi wa kesho atasonga mbele.
Katika hatua nyingine, Msuva alisema kuondoka kwake Yanga hakutaacha pengo kutokana na usajili wa Ibrahim Ajib, huku akisema kuwa mshambuliaji huyo ni mchezaji ambaye anacheza kama yeye  na ana  vitu vya ziada.