Wambura atoa ushahidi kesi ya akina Jamal Malinzi

Muktasari:

  • Akitoa ushahidi kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, Wambura alidai kwa sababu alikuwepo katika kikao hicho cha Juni 5, 2016 na hakukuwepo na ajenda ya kubadilisha watia saini wa benki wa TFF kwa kumtoa Edgar Masoud na kumuingiza Nsiande Mwanga.

OFISA Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), Boniface Wambura jana Jumatatu ametoa ushahidi wake na kuieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Muhtasari wa Juni 5, 2016 uliokuwa na ajenda ya kubadilisha watia saini wa akaunti za benki za TFF zilizopo Stanbic ni wa kughushi na kwamba yeye haufahamu. Wambura ambaye ni shahidi wa pili wa upande wa mashtaka aliyaeleza hayo wakati akiongozwa na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro kutoa ushahidi wake katika kesi inayomkabili aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi na wenzake wanne.

Akitoa ushahidi kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, Wambura alidai kwa sababu alikuwepo katika kikao hicho cha Juni 5, 2016 na hakukuwepo na ajenda ya kubadilisha watia saini wa benki wa TFF kwa kumtoa Edgar Masoud na kumuingiza Nsiande Mwanga.

Alidai, Edgar Masoud alikuwa ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala TFF lakini alifariki mwaka 2017.

Wambura alidai mchakato huo ulitakiwa kupelekwa kama ajenda ukieleza sababu za kutaka kufanya mabadiliko ya watia saini katika Kamati ya Utendaji ambapo ikiridhia mabadiliko hayo yanafanyika. Awali shahidi huyo alidai amekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu TPLB tangu Juni 2015 na kazi yake ni kusimamia ligi pia ni mjumbe Sekretarieti ya TFF. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 28 na 29 kwa ajili ya ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.