VIDEO: Simba yaondoka kwa mafungu Uturuki

Muktasari:

  • Waliondoka leo ni kocha msaidizi Mrundi Masoud Djuma, Meneja Richard Robert, Yassin Gembe (Daktari), Mwalami Mohammed (kocha wa makipa).

Dar es Salaam. Msafara wa kwanza wa Simba kwenda Uturuki umeondoka na viongozi wote wa benchi la ufundi kasoro kocha Patrick Aussems atakayeambana na wachezaji kesho asubuhi.


Waliondoka leo ni kocha msaidizi Mrundi Masoud Djuma, Meneja Richard Robert, Yassin Gembe (Daktari), Mwalami Mohammed (kocha wa makipa).
Viongozi hao waliwasili uwanjani wa ndege saa 7:30 mchana na waliondoka na Shirika la ndege la Emirates ambapo watakwenda mpaka Dubai kisha wataunga ndege hadi Uturuki.


Akizungumza akiwa uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, kocha Djuma alisema walifanya kikao na bosi wao mpya na kujadili mambo mengi ya msingi kubwa ilikuwa ni kupanga mipango ya kuhakikisha timu inafanya vizuri msimu huu katika mashindano yote.


"Ni mambo ya siri, lakini anaonekana ni kocha mwenye kiu ya kutaka mafanikio jambo ambalo hata mimi nalipenda nahaidi tutashirikiana nae na kuhakikisha timu inafika mbali zaidi ya msimu uliopita," alisema Mrundi huyo.  
"Tumewahi mapema katika safari hii si kama tunaondoka kwa makundi bali ni kuandaa mazingira ya timu itakapofikia na mambo mengine yote muhimu ambayo yalikuwa lazima tuanze kufika sisi kwanza.


"Tunafanya yote haya ya kwenda kuweka kambi nje ya nchi ili wachezaji kuhisi uongozi unataka wawepo katika mazingira salama ya kufanya maandalizi ili wakirudi nchini wanione kama wanadeni ambalo wanatakiwa kulilipa kwa kupata matokeo mazuri," alisema Djuma.


"Niwapongeze viongozi wamefanya jambo sahihi kutupeleka Uturuki kwani ni sehemu ambayo kama benchi la ufundi tumlizika nayo kwa asilimia zote, " aliongeza Djuma.
Meneja wa Simba, Richard Robert alisema kikubwa ambacho kilizungumzwa ni kujadili jinsi gani wachezaji wanatakiwa kufanya na ambaye atakuwa tofauti naye hawatakwenda sawa, lakini naimani wameelewana na kilichobaki ni utekelezaji tu.
"Wachezaji wote wa Simba na kocha Patrick wanafika uwanja ndege  saa 7:00 usiku na watapanda ndege ya moja kwa moja mpaka Uturuki ambapo tutakuwa tumeshawaandalia kila kitu muhimu maana tutafikia sehemu moja, " alisema Robert.