VIDEO: Kocha ngumi za Taifa anataka sifa aisee!

MMEMSIKIA Kocha wa timu ya Taifa ya ngumi za ridhaa? Huyu jamaa Benjamin Oyombi, hataki mzaha kabisa kwani, kawaambia mabondia wake wajiandae kwa lolote kwani atawafanyisha tizi hata kwenye ndege wakiwa safarini kwenda Australia katika Michezo ya Madola.

Oyombi mwenye leseni ya ukocha ya nyota tatu inayotambuliwa na Shirikisho la Ngumi za Ridhaa (AIBA) amesisitiza kutoka na ratiba yao kubana, mabondia hao wanaoongozwa na nahodha, Suleiman Kidunda hawatakuwa na muda wa kupoteza.

“Hata kwenye ndege kama itawezekana tutafanya mazoezi, hatuna muda wa kupoteza tena,” alisema kocha huyo baada ya kuuliza lini timu itaagwa na kuondoka kwenda Australia. Mpaka juzi Jumanne hakuwa na ratiba kamili ya safari yao.

Oyombi alipoambiwa timu itaagwa Machi 27 na itaondoka Machi 29 akaguna na kutamka kuwa siku ya kuagwa ndipo atakuwa na programu kali zaidi ya mazoezi.

“Ratiba iko ‘taiti’ mno, lakini sitapangua mipango yangu, nitawambia mabondia wangu wajiandae kwa lolote ikiwezekana hata kufanya mazoezi kwenye ndege tutafanya tu kwa kuwa sihitaji kupoteza muda,” alisisitiza kocha huyo na kufafanua.

“Nilishawahi kuifanyisha timu ya taifa ya Kenya ya vijana mazoezi ndani ya meli, tukiwa njiani tunakwenda katika Michezo ya Madola kwa vijana. Hivyo sio ishu kwangu kama nahitaji mafanikio,” alisisitiza kocha huyo raia wa Kenya.

Alisema anajua, ataalaumiwa timu itakapofanya vibaya kitu ambacho hataki kuona kinatokea na kusisitiza kwa idadi ya mabondia wanne wanaokwenda kuna medali moja.

“Idadi ni ndogo, katika hesabu za makocha uwa tunaamini unapopeleka mabondia 10 basi una hakika wa kurejea na medali tatu, nitakuwa na mabondia wanne Australia, natamani wote wafanye vizuri na ninajua wanaweza lakini natoa nafasi moja ya medali, tukipata nne ni faraja zaidi kwetu,” alisema.

Timu hiyo imepiga kambi Mkuza nje kidogo ya mji wa Kibaha , Pwani ambako Mwanaspoti iliitembelea na habari zaidi juu ya kambi hiyo. Jiandae kusoma makala juu ya kambi hiyo kesho Ijumaa.