VIDEO: Kerr apagawa na Gor! Ajichora tatoo ya klabu

Muktasari:

Kocha huyo alichora nembo hiyo katika duka moja la kucholea tatoo jijini Nairobi na zoezi hilo lilichukua takribani dakika 40 tu kumalizika.

Nairobi. Kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerr jana Jumatatu alijichora Tattoo yenye nembo ya klabu yake ya sasa  Gor Mahia ya Kenya katika mguu wa kushoto ikiwa ni ishara ya mapenzi yake baada ya kuiongoza kutwaa ubingwa wa Kenya.
Kocha huyo alichora nembo hiyo katika duka moja la kucholea tatoo jijini Nairobi na zoezi hilo lilichukua takribani dakika 40 tu kumalizika.
Mtaalamu wa kuchora Tattoo, Mark Moseti alisema alimchora nembo ya wastani, ambayo ilimgharimu kocha huyo kiasi cha 110,000 ya Tanzania.
Kocha Kerr alisema sababu kuu ya kuchora Tattoo ni kuweka kumbukumbu ya kuongoza Gor Mahia a.k.a Kogalo kutwaa ubingwa wa msimu wa 2017.
“Niliahidi jambo hilo miezi miwili iliyopita kwamba ningejichora iwapo tungeshinda taji. Nina Tattoo tatu kwenye mwili wangu, mbili za soka na moja ya mama yangu Gloria, ambaye atafika nchini (Kenya) wiki hii,” Kerr aliliambia Mwanaspoti.
“Ningependa kutunza kumbukumbu ya kutwaa ubingwa wa Kenya  katika maisha yangubila kujali nipo hapa au sipo. Si kila kocha anaweza kufikia mafanikio haya, makocha kadhaa wamepita katika klabu hii, baadhi wameshinda mataji na wengine wameshindwa."  
Kerr ana jumla ya mataji sita akiwa kama mchezaji na mawili akiwa kama kocha. Alishinda taji la Vietnam Cup na klabu cha Hai Pong mwaka 2014.
Tangu alipoanza kuinoa Kogalo kuchukua mikoba ya  Mbrazili Jose Marcelo Ferreira Julai 10, Kerr ameongoza Gor kwenye mechi 18 akishinda 14, katoa sare tatu na kupoteza moja tu dhidi ya Mathare United Oktoba 10.
Ubingwa wa msimu huu ni wa 16 kwa Kogalo, mataji matatu mbele ya watani wao wa jadi AFC Leopards na manne zaidi ya Tusker FC, ambao walishinda la mwaka jana.
Ingwe mwisho ilishinda ubingwa mwaka 1998 wakati huo straika wa zamani wa Yanga Boniface Ambani akiwa kwenye kikosini.