VIDEO: Duh! Hii kali Kagera yashangilia kufungwa Copa Umisseta

Muktasari:

  • Mashabiki na wachezaji wa Kagera walilipuka kwa furaha mara baada ya filimbi ya mwisho ya kumalizika kwa mchezo huo baada ya kufungwa magoli 45-15 katika mchezo wa netiboli dhidi ya Morogoro kwenye viwanja vya Chuo cha Ualimu Butimba.

Mwanza. Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya firauni, hicho ndicho kimetokea kwa timu ya mkoa wa Kagera pamoja na kupokea kipigo ndiyo waliolipuka kwa shangwe katika moja ya mechi za mashindano ya Copa Umisseta.


Mashabiki na wachezaji wa Kagera walilipuka kwa furaha mara baada ya filimbi ya mwisho ya kumalizika kwa mchezo huo baada ya kufungwa magoli 45-15 katika mchezo wa netiboli dhidi ya Morogoro kwenye viwanja vya Chuo cha Ualimu Butimba.


Pamoja na kipigo hicho, Kagera walishangilia kwa mbwembwe takribani dakika 20 huku timu iliyoshinda ikionyesha kunyong'onyea kama kwamba imefungwa.


"Hawa Morogoro walituambia wakituonea huruma basi watatufunga magoli 50, lakini hawajayafikisha, hicho ndicho kimetupa furaha mno," alisema kocha wa Kagera, Joyce Kisike.


Wachezaji wa timu ya Kagera na mashabiki wao walizunguka viwanja vya chuo hicho wakishangilia licha ya kipigo walichopata wakidai kipigo hicho ni ushindi kwao kwani wamecheza na timu ya akademia ambayo walijua watafungwa magoli hata 100, lakini wameikazia.