BADO WAMO: Uzazi haujawahi kuwafunika aisee

Jacqueline Mengi

LILE shindano la urembo ndio kama ulivyosikia. Ndiyo, Miss Tanzania kwa sasa ni kama imekufa na wale waandaaji waliozoeleka wameshalitema. Lilianza kupigwa na dhoruba ya malalamiko ya upangaji matokeo kutoka kwa washiriki na wadau wa fani hiyo kwa jumla kisha ikaibuka ishu ya zawadi.

Hata hivyo, historia inaturudisha nyuma kabisa wakati shindano hilo lilipokuwa moto kwelikweli kutokana na mvuto na uzuri wa washiriki wa miaka hiyo.

Ndiyo, si unawakumbuka Faraja Kota, Nancy Sumari, Irene Kiwia, Happiness Magese, Mercy Galabawa, Nargis Mohamed, Wema Sepetu, Jacqueline Ntuyabaliwe na Joketi Mwegelo mambo yalikuwa ni moto.

Kwa sasa warembo hao waliopata kutamba na kuiletea sifa Tanzania kwenye fani ya urembo, wamejiweka pembeni wakiendesha familia zao baada ya kuolewa na wengi wamepata watoto.

Lakini, ishu ambayo imeendelea kuwa gumzo kwenye fani hiyo ni warembo hao licha ya kuwa na watoto, wamezidi kuwa na mvuto zaidi machoni mwa watu kiasi cha mashabiki kupagawa kila wanapowaona.

Hebu kwa uchache angalia warembo hawa ambao, hata wakiamua kushikiri shindano la Miss Tanzania sasa hivi wana uwezo mkubwa wa kushinda licha ya kuwa ni wakongwe.

NANCY SUMARI

Tanzania imeshiriki sana mashindano ya urembo ya kimataifa, lakini mwaka 2005 ilianza kufurahia matunda baada ya Nancy Sumari kuandika historia kwenye fani ya urembo.

Kutoka kuwa wasindikizaji hadi kunasa taji la Miss World Africa, ambalo mrembo huyo aliyekuwa Miss Tanzania 2005 alishinda kwenye Miss World.

Baada ya kushinda taji hilo, Nancy aliendelea kukuza fani hiyo ya urembo kimataifa huku akitumika kuwafunda warembo waliokuja nyuma yake. Lakini, Julai 2016 mrembo huyo alifunga ndoa na mpenzi wake Luca Neghesti mwenye asili ya India. Neghesti ndiye Mwenyekiti Mtendaji wa Bongo5 Media Group Ltd huku Nancy akiwa Mkurugenzi.

Hata hivyo, kabla ya ndoa hiyo, wawili hao tayari walijaliwa kupata mtoto wa kike, Zuri.

Pamoja na kujifungua huko mwili na hata sura yake havijabadilika hadi leo na anaweza kurudi jukwaani na kuchuana na warembo wengine wachanga katika masuala ya urembo, licha ya kanuni za mashindano ya urembo haziruhusu mshiriki ambaye tayari amejifungua.

Jacqueline Mengi

Miaka hiyo wengi walimtambua kama Jacqueline Ntuyabaliwe, lakini kwa sasa kila kitu kimebadilika. Mrembo huyo mwenye mvuto wa aina yake kwa sasa ni mke wa Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi. Jacqueline, Miss Tanzania mwaka 2000, pia ni mwanamitindo na msanii mahiri wa muziki nchini na alikuwa akifahamika kama K-Lyinn wakati huo akitamba na hit zake kibao ikiwemo Nalia kwa furaha katika albamu yake ya Crazy Over You.

Machi 2015, mrembo huyo alifunga ndoa na Mengi wakati huo tayari wakiwa wamejaliwa kupata watoto mapacha.

Kama mnavyojua wakwe wa kichaga wanavyojua kulisha wazazi hususani vyakula kama supu, uji, mtori unaosindikizwa na nyama, bado mrembo ameweza kulinda shapu yake ya kimiss na kumfanya kuwa bomba zaidi.

Kwa sasa Jacqueline ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa nchini, akimiliki biashara mbalimbali ikiwemo kampuni ya kutengeneza thamani za majumbani na ofisini ya Amorette.

Faraja Kotta

Ni nadra sana kusikia aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini kupitia CCM, Lazaro Nyalandu, akimuita Miss Tanzania 2004 kwa jina la Faraja. Mara nyingi utasikia Far au mama Sarah. Ndio, Faraja Kotta aliibukia Miss Ubungo kisha Kinondoni na baadaye kubeba taji la Miss Tanzania.

Tena warembo wa Tanzania miaka hiyo walikuwa wakinasa dili za maana na ndinga kali kama zawadi kwa kubeba taji hilo tofauti na miaka ya hivi karibuni, ambapo zawadi ilikuwa utata kwelikweli.

Novemba 30, 2007, Nyalandu alimbeba jumla Faraja na kuwa mkewe halali na kwenye ndoa hiyo wamebarikiwa watoto wawili mpaka sasa, Christopher na Sara.

Lakini, jambo la kufurahisha zaidi ni kuwa Faraja mpaka sasa bado ana vigezo vyote vya urembo na sura yake bado inakimbiza kwelikweli.

Kwa sasa Faraja na muasisi na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Shule Direct, ambayo imekuwa ikijihusisha na mpango wa kuwasaidia wanafunzi kupata elimu ya masuala ya fedha na utunzaji wa kumbuku za fedha.

Irene Kiwia

Unamkumbuka Irene Kiwia? Ndio yule ambaye alileta staili ya kukata nywele na kubaki kama kipara vile. Wakati warembo sasa hivi wakiona ndio staili ya kijanja, Kiwia alishatesa nayo kitambo tu na sasa amebadili muonekano wake kidogo tu.

Ni miongoni mwa rembo wachache nchini waliopeperusha vyema bendera ya Tanzania kwenye mashindano ya urembo kimataifa, baada ya kunyakuwa taji la ‘Face of Africa’.

Kiwia, ambaye aliwahi pia kubeba taji la Miss Temeke mwaka 2000, ambapo mwaka huo alimaliza kwenye tatu bora ya Miss Tanzania.

Mrembo huyo ana watoto watatu, Zion aliyemzaa Julai 9, mwaka 2005, Ethan na Axelle aliyejifungua Mei mwaka 2015, lakini bado yuko bomba na analipa kwelikweli.

Kama ilivyo kwa wenzake, Irene anamiliki kampuni inayojishughulisha na mawasiliano na matangazo ya Frontline Porter Novelli.

Happiness Magese

Baada ya kuteseka kwa muda mrefu, bila ya kupata mtoto hatimaye mwaka jana, mwanamitindo Happiness Millen Magese, alijaliwa zawadi hiyo kutoka kwa Mungu.

Millen, ambaye aliwahi kuwa Miss Tanzania mwaka 2001 na baadaye kujikita katika uanamitindo na kuitangaza vema Tanzania kimataifa, alipata mtoto wake wa kwanza Julai mwaka jana.

Kwa nyakati tofauti, amewahi kusimulia na kumwaga machozi akielezea tatizo lake la kutoshika ujauzito kutokana na mirija yake kuziba.

Kwa sasa amefanikiwa kupata mtoto wa kiume na kumpa jina la Prince Kairo Michael Magese na bado anaonekana mrembo wa nguvu mpaka sasa.

Mwaka 2014, Millen alianzisha mfuko kwa wanawake kwa ajili ya kutibu matatizo ya uzazi, ugonjwa ambao uliomsumbua kwa miaka mingi huku lengo lake likiwa ni kusaidia kuelimisha wanawake ili kujua dalili na matibabu ya ugonjwa huo.

Daktari aelezea sababu

Daktari bingwa wa wanawake na watoto, Dk. Willy Sangu, anasema ili mwanamke aweze kubaki na umbo lake kama alivyokuwa kabla hajajifungua, anatakiwa kuwa msafi hususani katika maeneo yake ya kizazi.

Pia, anatakiwa kuzingatia vyakula vilivyo na virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini na hapa anasisitiza sio kula sana kwa kisingizio kuwa unanyonyesha na kudai kwamba, hapa ndipo wanawake wengi wanapoharibu mambo.

“Utakuta mzazi unakula vyakula vya wanga kuanzia asubuhi mpaka jioni au vyakula vyenye mafuta mengi ambapo, wengi wanadanganyana vinasafisha tumbo, hakuna kitu kama hicho zaidi ya kujiongezea unene na uzito usio na tija,” anasema.

Kwa mujibu wa Dk. Sangu, jambo lingine muhimu la kuzingatia ni kufanya mazoezi kwa wingi ambapo, wataalam wa mazoezi wanaweza kumuelekeza mama aina ya mazoezi yanayofaa na kwa wakati wake hata kama umefanyiwa operesheni.

Kuhusu mwanamke aliyefanyiwa operesheni kama sindano anazochomwa kuwa ndio zinachingia kumnenepesha, Dk. Sangu amepinga madai hayo na kueleza halina ukweli ni mambo ya kujiendekeza tu na kukaa bila kufanya mazoezi.

“Hakuna ukweli hapa, ndio sababu mzazi anayejifungua kwa upasuaji siku ya pili baada ya dawa za usingizi kumuisha, anashauriwa kufanya mazoezi. Hapa ataanza kufanya mazoezi madogo madogo madogo hadi miezi mitano au sita na atakuwa akishiriki kawaida kama wengine. Hayo mengine wapuuze kama wanataka kulinda muonekano wao,” alisisitiza.