Ukitoka kuiona Yanga hamia pale jirani tu

Muktasari:

Fainali hiyo ya wanaume itapigwa Uwanja wa Ndani wa Taifa ulio jirani kabisa ya dimba la Uhuru, mwendo wa dakika tano tu na itaanza saa 2:00 usiku kwa kuzikutanisha JKT iliyokuwa ikisubiri bingwa kati ya Oilers na Savio waliocheza jana Ijumaa usiku.

MECHI ya Yanga na Ndanda FC ya Ligi Kuu Bara inachezwa jioni ya leo Jumamosi Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, lakini ikimalizika tu, hapo jirani kuna fainali ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam na bingwa atapewa medali ya dhahabu, Sh700,000 na kombe juu.

Fainali hiyo ya wanaume itapigwa Uwanja wa Ndani wa Taifa ulio jirani kabisa ya dimba la Uhuru, mwendo wa dakika tano tu na itaanza saa 2:00 usiku kwa kuzikutanisha JKT iliyokuwa ikisubiri bingwa kati ya Oilers na Savio waliocheza jana Ijumaa usiku.

Msemaji wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam, Peter Mpangala, alisema mshindi wa pili atapewa medali ya fedha na Sh500,000 na mshindi wa tatu atazawadiwa medali ya shaba na Sh300,000.

Kwa mujibu wa Mpangala, zawadi hizo zitatolewa pia kwa wanawake na mechi zitaanza saa nane mchana kwa kusaka mshindi wa tatu upande wa wanawake kabla ya fainali itakayozikutanisha Don Bosco Leoness na Vijana Queens, saa 10 jioni.

Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.