Uchukuaji fomu za uchaguzi Simba siri tupu

Muktasari:

  • Uchukuaji wa fomu ulikuwa ukifanyika makao makuu klabu ya Simba mtaa wa Msimbazi lakini kulikuwa na mwitikio mdogo wa wanachama kuchukua fomu hizo.

Dar es Salaam. Kamati ya uchaguzi ya Simba imetoa kali baada ya kushindwa kuweka bayana majina na idadi ya wanachama waliojitokeza kuchukua fomu hadi wakati wanafunga saa 10:00 jioni ya leo Jumatatu.

Uchukuaji wa fomu ulikuwa ukifanyika makao makuu klabu ya Simba mtaa wa Msimbazi lakini kulikuwa na mwitikio mdogo wa wanachama kuchukua fomu hizo.

Katibu wa kamati ya uchaguzi wa Simba, Arnold Kashembe aliyekuwa akisimamia uchukuaji wa fomu hizo hadi muda wa mwisho wa kuchukua fomu unafika alikataa na kugoma kutangaza wagombea walijitokeza.

"Siwezi kutangaza wala kusema wagombea ambao walichukua fomu kwani hilo siyo jukumu langu," alisema Kashembe.

"Muda ukifika mtatangaziwa, lakini kwa sasa mimi sina mamlaka ya kusema lolote mpaka hapo tutakapomkabizi Mwenyekiti ya kamati ya uchaguzi majina ya waliochukua fomu na yeye ndio atasema hadharani," aliongezea Kashembe.

Katika makao makuu ya Simba nje walikuwa wapenzi na mashabiki waliokuwa wakisikilizia labda huenda kuna mgombea angetangazwa kama amekuja kuchukua fomu, lakini mpaka ofisi zinafungwa halikufanyika jambo hilo.

Mmoja wa mashabiki aliyekuwa karibu na Kashembe aliidokeza kile ambacho alikiona kwa wale ambao wamechukua fomu.

"Nimeona baadhi ya majina katika nafasi ya Mwenyekiti wamejitokeza wawili ambao ni Mtemi Ramadhani na Sweedy Mkwabi," alidokeza shabiki huyo ambaye alikataa kutaja jina lake.

Majina mengine yaliyohusishwa kwa kunyapia nyapia ni Patrick Lweimam, Asha Baraka, Mwina Kaduguda, Jasmin Badru, Ally Sulu, Iddy Kajuna, Said Tully, Amiss Ramadhani, Abdallah Migomba na Alfred Eliya.

Wakati mashabiki hao wakiwa wanajiandaa kuondoka ghafla walianza kupiga shangwe la kelele kuwa Salim Abdallah 'Try Again' mbali ya kukataa kuchukua fomu lakini kuna mtu alikuja kumchukulia.

"Tumepata taarifa sasa kuwa Try Again ameshachukuliwa fomu tayari ndio maana tunafurahi na kuondoka kwa amani kwani hilo ndio tulikuwa tunalitaka," walisema mashabiki hao.