Ubabe wa Simba na Yanga Kwenye Soka Letu

Muktasari:

Siyo kwamba hawakumpenda au aliwafunga sana, la hasha. Sir Alex alipendwa na wengi kuliko waliomchukia. Na hata waliomchukia, hawakufanya hivyo kwa kumlenga yeye kama binadamu bali kama kocha wa klabu kubwa na yenye mafanikio zaidi kwenye soka la nchi hiyo.

WAKATI Sir Alex Ferguson anatangaza kustaafu kufundisha soka, watu wengi kwenye mamlaka za soka England, kasoro wa Manchester United, walifurahi kutokana na uamuzi huo.

Siyo kwamba hawakumpenda au aliwafunga sana, la hasha. Sir Alex alipendwa na wengi kuliko waliomchukia. Na hata waliomchukia, hawakufanya hivyo kwa kumlenga yeye kama binadamu bali kama kocha wa klabu kubwa na yenye mafanikio zaidi kwenye soka la nchi hiyo.

Watu wengi walifurahi kwa sababu waliamini kwamba ‘sasa nchi ilikuwa ikielekea kupata uhuru’ kutoka kwa ‘mkoloni’ Ferguson. Fergie alikuwa mkoloni wa soka la England, alikuwa na nguvu zisizomithilika. Alikuwa dikteta!

Fergie aliwapiga marufuku baadhi ya waandishi kwenda Old Trafford, mmoja wao ni Daniel Taylor wa gazeti la The Guardian. Fergie aliwapiga marufuku BBC kuzungumza naye kwa lolote, tangu 2004 mpaka 2011 pale mkurugenzi mkuu Mark Thompson alipoenda kumbembeleza ‘babu’.

BBC ni moja ya vyombo vya habari vyenye haki ya kuonyesha EPL na Sheria za FA zinawataka makocha wote wawe tayari kuongea na vyombo vyote vyenye haki, Fergie akakaidi kwa miaka saba na FA ikamuogopa.

Mwaka 2010, mtoto wake, Darren Ferguson, alikuwa kocha wa Preston North na Ferguson aliwapeleka wachezaji wake watatu (Ritchie de Laet, Joshua King and Matty James) kwa mkopo kwenye klabu hiyo. Kutokana na matokeo mabaya, mwanaye akafukuzwa, hapo hapo Ferguson akawachukua wachezaji wake wawili kati ya watatu aliowapeleka kwa mkopo, halafu akafungua kesi kutaka yule watatu aliyebaki asiichezee kabisa klabu hiyo.

Wakati klabu hiyo ikihangaika kuziba pengo la wachezaji hao, ikakutana na pigo jingine pale wachezaji wengine wawili, Danny Pugh na Michael Tonge, waliokuwa kwa mkopo kutoka klabu ya Stoke City, walipochukuliwa ghafla kurudi kwenye klabu yao. Kocha wa Stoke City wakati huo alikuwa Tony Pullis ambaye ni rafiki mkubwa wa Sir Alex Ferguson. Alifanya hilo kwa ajili ya Fergie? Wanajua wenyewe. Mwamuzi mmoja, Jeff Winter, aliwahi kutoa ushuhuda kwamba aliadhibiwa na FA kwa kunyimwa kuchezesha mechi za Man U kwa miaka miwili. Akaongeza kwamba FA huogopa kumpa tena mwamuzi mechi za Man U endapo aliwahi kukosolewa na Ferguson.

Huyu alikuwa Ferguson. Waamuzi walimuogopa. FA ilimuogopa. Waandishi walimuogopa. Mpaka vilabu vilimuogopa. Kwa hiyo alipostaafu, hawa wote walifurahi.

TURUDI KWENYE MADA

Nimeanza kwa kuelezea nguvu alizokuwa nazo Alex Ferguson kwenye soka la England ili kutengeneza mazingira ya kueleweka nitakachokieleza.

Hapa nchini, hakuna mtu mwenye nguvu za namna hiyo katika soka, bali nguvu hizo zimewekezwa kwenye klabu, hasa mapacha wa Kariakoo, Simba na Yanga.

Klabu hizi zimepewa nguvu na mifumo yetu ya soka kiasi cha kuweza kufanya chochote kwenye mpira wetu. Vimepewa nguvu kiasi cha kuogopwa na waandishi na vyombo vya habari kwa ujumla, waamuzi na hata vilabu vingine na hata makocha. Lakini mbaya zaidi, hata FA yetu (TFF) inaziogopa klabu hizi kiasi cha kushindwa kufanya uamuzi sahihi kwa faida ya mpira wetu.

Niliangalia mchezo wa Jumapili ya Aprili 15 kati ya Azam FC na Njombe Mji kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi. Njombe Mji walifunga bao halali lakini mwamuzi ‘dada’ Jonesia Rukya akalikataa. Azam FC walipata penati halali lakini nahodha ‘Ninja 23’ Himid Mao akakosa.

Wakati dada akipuliza kipenga cha mwisho kumaliza mchezo huo, picha iliyonijia kichwani ni kwamba yawezekana matokeo haya yalikuwa mipango ya Mungu kuonesha namna gani timu hizi zinavyolingana. Machi 11, Mjombe Mji walitakiwa kucheza na Simba lakini ratiba ikabadilishwa ili kuipa Simba nafasi ya kujiandaa na mchezo wa kimataifa dhidi ya Al Masry wa Machi 17.

Kiporo hicho kikapangwa kufanyika Aprili 3, siku chache baada ya Njombe Mji kucheza na Stand United kwenye robo fainali ya kombe la FA, Machi 30.

Mchezo huu uliahirishwa ili kuipa nafasi Simba kujiandaa kimataifa lakini ukapangwa kufanyika katika siku ambayo Njombe Mji hawakupewa nafasi ya kujiandaa. Shida ya Simba, wakaadhibiwa Njombe Mji.

Jaribu kufanya kinyume chake, kwenye Njombe iweke Simba na kwenye Simba iweke Njombe, halafu panga ratiba kama hiyo…THUBUTU!

Azam FC waliingia kwenye mchezo dhidi ya Njombe Mji wakitoka kucheza na Ruvu Shooting katika mchezo uliolala kutokana na mvua. Kanuni za FIFA zinataka wachezaji angalau wapate saa 72 za kupumzika kabla ya mchezo mwingine. Lakini kwa Azam FC, hazikufika saa 72 kutoka mchezo na Ruvu Shooting hadi dhidi ya Njombe Mji.

Bahati nzuri ni kwamba Azam iliandika barua kuomba mechi hiyo isogezwe lakini hakuna aliyesikia kilio chao. Nani anajali sana kuhusu Azam? Hakuna.

Jaribu kuwaweka Yanga kwenye nafasi ya Azam FC halafu panga ratiba kama hiyo ya kucheza baada ya siku mbili uone moto wake.

Yanga na Simba zimeachwa kuwa madikteta wanaoutawala mpira wa hapa nchini. Katika mazingira kama haya, ni bora udikteta wa Sir Alex Ferguson kwa sababu una mwisho. Alipoondoka, akaondoka nao. Lakini udikteta wa kitaasisi hauna mwisho...kwa kadiri mnavyozidi kuuchekea, na wenyewe unazidi kukua. Hispania wanajua ubaya wa kuendekeza udikteta wa klabu kama tunaouchekea hapa. Real Madrid na FC Barcelona ziliachwa zikatawala La Liga kiasi kwamba mapato ya haki za TV, wao peke yao wanachukua nusu halafu iliyobaki ndiyo kwa zingine 18.