Julio ataka timu za jeshi zipungue

Muktasari:

Akizungumza baada ya mchezo huo uliolazimika kumalizikia ‘gizani’ Julio alisema uwepo wa timu za majeshi unaleta wasiwasi mkubwa sana kwa timu pinzani na waamuzi wanaochezesha mechi dhidi ya timu hizo.

 Licha ya timu yake Dodoma FC kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Oljoro, kocha Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’ ameliomba Shirikisho la Soka nchini {TFF} kuzipunguza timu za majeshi kama ilivyofanyika kwa timu za Polisi.

Akizungumza baada ya mchezo huo uliolazimika kumalizikia ‘gizani’ Julio alisema uwepo wa timu za majeshi unaleta wasiwasi mkubwa sana kwa timu pinzani na waamuzi wanaochezesha mechi dhidi ya timu hizo.

“Nashukuru tumepata ushindi muhimu na hatimaye tumekaa kileleni kuongoza kundi letu ila kilio changu naomba TFF waufanyie kazi kuhusiana na timu za majeshi zinatupa uoga timu zetu za kiraia na ikiwezekana wabaki na timu moja kama walivyofanya Polisi,” alisema Julio.

Naye kocha wa Oljoro JKT ya Arusha, Emmanuel Massawe alizipeleka kwa mwamuzi Said Pambalelo wa Dar es Salaam kuwa ndiye sababu za timu yake kufungwa.

“Sioni tatizo kwa timu wala wachezaji wangu kwenye mchezo huu badala yake namlaumu mwamuzi wa mchezo huu kwa kuuharibu mchezo wote kwa kuchezesha vibaya na kusababisha timu yangu kufungwa” alisema Massawe

Katika mchezo huo bao la ushindi wa Dodoma FC lilifungwa na kiungo Rajab Mgalula aliyefunga kwa ‘tik tak’ ilishuhudiwa ukimalizika gizani kutokana na matukio kadhaa likiwemo la kuchanwa kwa nyavu za goli la kusini lililochukua zaidi ya dakika 5 kuziweka sawa.