Tamthilia ya Mourinho, Pogba utaipenda

Muktasari:

Wawili hao inasemaka hapo katika maelewano mazuri katika siku za karibuni

Manchester, England. Suala la kiungo ghali wa Manchester United, Paul Pogba kutaka kuondoka limeendelea kuwa kama tamthilia inayoibua mapya kila uchao, baada ya kocha wa timu hiyo Jose Mourinho, kusema hataki tena kusikia neno kuondoka.

Mourinho anadaiwa sababu ya Pogba kutaka kuondoka Old Trafford kutokana na kumshutumu kila mara nyota huyo wa Ufaransa kwamba hajitumi anapoitumikia timu hiyo, amepinga akisema anaishi naye vizuri na hawana tofauti yoyote.

Alisema yeye anamthamini na anampenda mchezaji huyo ndiyo maana aliamua kumrudisha United kwa kumnunua kwa dau nono mwaka 2016 kutoka Juventus ya Italia.

“Ninakasirika kwa sababu hamtaki kumuachia Pogba acheze mpira, kila siku kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii habari kuu ni ya Pogba kuondoka United, mimi hajaniambia hata mara moja kuwa hana raha hapa au anataka kuondoka, tangu amerudi kutoka kwenye fainali za Kombe la Dunia nimekuwa naye na tunafanya kazi vizuri,” alisema Mourinho na kuongeza.

“Sitaki tena kuzungumzia suala hili, nitazungumza kile ambacho nimekisema lakini sio kile nilichokisoma, siwezi kupasuana vichwa na watu ambao hawakubali ninayoyasema bali wanataka yale wanayoyasikia kwingine, Pogba hajawahi kuniambia anataka kuondoka,” alisema.

Alisema kinachozungumzwa kila siku kuhusu Pogba kina madhara makubwa kwa mchezaji huyo na kwa klabu pia, huku akisisitiza kuwa hatandoka hadi mwisho wa mkataba wake utakaomalizika mwaka 2021.

Mchezaji huyo ameshakiri mara kadhaa kuwa hana furaha ila hayupo huru kuzungumza kila kilicho moyoni mwake kwa kuwa ataadhibiwa, kabla ya dirisha la usajili wa kiangazi kufungwa, alifanya mazungumzo na Barcelona, ingawa klabu hiyo iliwasilisha ofa mara mbili zilikataliwa na United, makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Ed Woodward, akisisitiza kuwa Pogba hauzwi.