Straika wa Asec kutua Yanga

Muktasari:

  • Katika muendelezo ule ule wa kuifanya Yanga iwe moto zaidi, Mkongo huyo amewasilisha ombi kwa mabosi wake akitaka aletewe straika matata, Ahmed Toure raia wa Burkina Faso anayekipiga Asec Mimosas ya Ivory Coast.

KAMA kuna kitu ambacho mashabiki wa Yanga wanacheka kwa sasa ni kazi nzuri iliyofanywa na Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Mwinyi Zahera katika kuwaletea wachezaji wa maana tangu atue Jangwani.

Katika muendelezo ule ule wa kuifanya Yanga iwe moto zaidi, Mkongo huyo amewasilisha ombi kwa mabosi wake akitaka aletewe straika matata, Ahmed Toure raia wa Burkina Faso anayekipiga Asec Mimosas ya Ivory Coast.

Kocha Zahera katika maombo yake aliwataka mabosi wake, kumletea straika mmoja au wawili wa maana, ili waungane na Heritier Makambo ndipo jina la Toure likaibuka na haraka Yanga wameanza mipango ya kumleta dirisha dogo.

Straika huyo mwenye miaka 31 akiwa na urefu wa futi 6 na inchi 2 na aliyewahi kukipiga Asante Kotoko ya Ghana alionwa na Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na jamaa anajua kucheka na nyavu.

Ingawa Yanga inafanya siri, lakini Mwanaspoti linafahamu kwamba Bosi wa Usajili Hussein Nyika amemtuma kigogo mmoja katika kamati yake kwenda kufanya mazungumzo na straika huyo aliyerudi klabu kwake akitoka kuitumikia taifa lake katika mechi za kimataifa wikiendi iliyopita.

Hata hivyo, upinzani mkubwa kwa Yanga ni kumshawishi mshambuliaji huyo kuikubali Yanga kuachana na ofa ya nchini Iceland aliyoipata ambapo moja ya klabu ya huko imemtaka kusubiri mpaka Novemba kumtumia tiketi aende huko.

Inaelezwa kwamba mbali na Toure kamati ya Nyika ina majina matano ambayo ndani yake kuna washambuliaji hatari kama alivyo Toure.

Taarifa hiyo ikalifanya Mwanaspoti kumsaka Toure na kuona makali yake ambapo kama akipata nafasi ya kufunga kwa mguu wa kulia au kichwa hakuachi.

Kufuatia taarifa hizo Mwanaspoti lilimtafuta Nyika kujua ukweli wa hilo ambapo alishindwa kukubali au kukataa akisema bado wanaendelea kukifanyia maboresho kikosi chao lakini kwasasa hawawezi kusema lolote juu ya Toure.

“Tunaendelea kufanya maboresho katika kikosi chetu lakini sio kila kitu kinatakiwa kutolewa kwanza hadharani, huyo Toure siwezi kuweka wazi chochote kwasasa,” alisema Nyika na kukata simu.

KINDOKI ASHUSHA FRESHA

Katika hatua nyingine, kipa wa Yanga Nkinzi Kindoki amewashusha presha mashabiki wa timu waliokuwa na hofu ya kumkosa uwanjani baada juzi Jumanne kuumia mazoezini na kushindwa kuendelea na wenzake.

Mkongo huyo alishindwa kuendelea na mazoezi kutokana na kushtua jeraha lake ya kifundo cha mguu.

Bahati nzuri, madaktari wa timu hiyo wamechangamka fasta na kumtibia na sasa jamaa karejea tena uwanjani na kushusha presha waliokuwa nayo makocha na hata mashabiki wa klabu hiyo yenye rekodi ya kubeba mataji 27 ya Ligi Kuu Bara.

Kindoki aliwateka mashabiki wa klabu hiyo kwa kazi kubwa aliyoionyesha katika pambano la kirafiki dhidi ya African Lyon, likiwa la kwanza kwake kulicheza jijini Dar es Salaam akiwa na Yanga iliyomsajili hivi karibuni. Yanga ilishinda bao 1-0.

Kuumia kuliwafanya mashabiki kuingiwa na hofu ya kumkosa kwenye pambano la Ligi Kuu Jumapili hii dhidi ya Stand United ya Shinyanga.

Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh aliliambia Mwanaspoti ni kweli Kindoki akuiumia na kushindwa kuendelea na mazoezi na wenzake, lakini hali yake kwa sasa sio mbaya kwani alishapatiwa matibabu.

“Kweli alipata majeraha, ila ni kawaida kwa mchezaji muda mwingine kushtua viungo vyake, amerejea mazoezini leo Jumatano (jana) baada ya kupata matibabu na anaendelea vizuri kama zamani,” alisema. Hafidh aliongeza wachezaji wengine wote wamerejea katika kikosi hicho, isipokuwa winga Juma Mahadhi anayesumbuliwa na majeraha ya goti.