Spurs yaivaa Real leo

Muktasari:

Real Madrid ni bingwa mara 10 wa Ligi ya Mabingwa Ulaya

London, England. Kocha wa Tottenham Hotspurs, Mauricio Pochettino, amesema mchezo wa leo dhidi ya Real Madrid utakuwa ni vita.

Pochettino alisema Real Madrid ni timu ngumu na Spurs itakuwa macho na wachezaji wote na siyo Cristiano Ronaldo.

Kocha huyo alisema Real Madrid ina wachezaji wote bora na mabeki wake hawatakuwa na kazi pekee ya kumpa ulinzi mkali Ronaldo.

Spurs itakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu kuikabili Real Madrid katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Timu hizo zinavaana zikiwa na pointi sita kila moja na mchezo wa leo utakuwa wa kukata na shoka kwa kuwa zinakabana koo katika Kundi H.

"Ronaldo ni mchezaji hodari sana muhimu kuchungwa, lakini wachezaji wote ni hodari. Kikosi kina kocha bora kinavutia," alisema Pochettino.