Sindano tano za moto England

ACHANA na nani atakuja kwenye vikosi vya Ligi Kuu England wakati dirisha la usajili likitarajiwa kufungwa leo Alhamisi, habari ya mjini ni hawa mastaa watano ambao wameshajiunga na vikosi vipya kwenye ligi hiyo.

Kuna majina ya wachezaji wengi waliobadili timu kwenye Ligi Kuu England, lakini wakali hawa watano, wataangaziwa macho zaidi kuona kitu gani watakifanya kweli ligi hiyo yenye ushabiki mkubwa duniani.

1.Riyad Mahrez (Man City)

Bila ya kujali kama Manchester City kweli ilihitaji huduma ya kiungo mshambuliaji au la, lakini ukweli Riyad Mahrez ametua Etihad na shughuli yake huwa si ya kitoto.

Kutokana na hilo, Man City sasa inakuwa na orodha ndefu ya wachezaji matata kwenye safu yake ya ushambuliaji kwa sababu Mahrez anakwenda kukutana na wakali kama Raheem Sterling, Bernado Silva, Leroy Sane, David Silva na Phil Foden.

Kwenye hilo, Pep Guardiola atakuwa kwenye wakati mgumu kwelikweli kupanga kikosi chake. Lakini, yote kwa yote ni kupata huduma ya bora kwenye kikosi chake.

2.Fred (Man United)

Staa wa Kibrazili, Fred ametua Old Trafford. Kiungo huyo ameripotiwa kuwa na vitu vingi adimu ambavyo mashabiki wa Manchester United wanaamini watakuwa kwenye wakati mzuri kumtazama mchezaji huyo.

Ujio wake huko Old Trafford utamfanya kwenye kucheza sambamba na Paul Pogba na Nemanja Matic, licha ya kuwapo kwa ripoti Pogba anaweza kutimkia Man United.

Hata hivyo, Man United haiwezi kukubali kumuuza Pogba kama haitakuwa imempata mrithi wake hasa ukizingatia dirisha lenyewe la usajili linafungwa leo Alhamisi.

3.Alisson (Liverpool)

Liverpool ilikubali tu kuweka rekodi ya kusajili kipa kwa pesa nyingi. Kocha Jurgen Klopp aliingia sokoni kumnasa kipa wa Kibrazili, Alisson Becker kutoka AS Roma na hakika jambo hilo limeipa matumaini makubwa ya kufanya vyema kwenye ligi ya msimu ujao.

Pesa nyingi zilitumika kunasa huduma yake na hakika ni moja ya wachezaji ambao wametua kwenye Ligi Kuu England na kutumainiwa watafanya mambo makubwa.

4.Jorginho (Chelsea)

Pep Guardiola alikuwa akimpigia hesabu kali sana za kumnasa akacheze kwenye kikosi chake cha Manchester City. Lakini, hilo lingetokea kama tu Chelsea isingekuwapo, kwani ilivamia dili hilo na kumbeba Jorginho kibabe.

Hivi unavyosoma hapa, kiungo huyo wa kati wa Kitaliano mwenye asili ya Brazi, ametua kwenye kikosi cha Chelsea chenye maskani yake Stamford Bridge akitokea Napoli. Pesa nyingi zimetumika kupata saini yake, lakini kinachosubiriwa ni kuona atakavyokwenda kutamba kwenye kikosi hicho cha The Blues chenye vichwa vingi matata akiwamo Cesc Fabregas, N’Golo Kante na Eden Hazard.

5.Richarlison (Everton)

Mbrazili Richarlison amekuwapo kwenye Ligi Kuu England ana ifahamu vyema ligi hiyo. Alikuwa na kiwango bora kabisa kwenye kikosi cha Watford na hilo lilitosha kumpa nafasi ya kutua Everton kwa pesa nyingi.

Kiwango cha Richarlison hakina shaka na ndiyo maana wakali hao wa Goodison Park wameshawishika kutoa pesa nyingi kuchukua huduma yake, ambapo sasa atakwenda kucheza pamoja na mastaa makini kama vile Theo Walcott.