Simba huko Uturuki mambo ni moto

Muktasari:

Simba imefikia katika hoteli ya The Green Park Kartepe Resort and Spa iliyopo katika jiji wa Istanbul Uturuki na watakuwa hapo kwa muda wa siku 16 na watarudi nchini Agosti 5 siku tatu kabla ya siku ya Simba (Simba Day).

Dar es Salaam. Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba wapo nchini Uturuki wakiendelea na mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.
Simba imefikia katika hoteli ya The Green Park Kartepe Resort and Spa iliyopo katika jiji wa Istanbul Uturuki na watakuwa hapo kwa muda wa siku 16 na watarudi nchini Agosti 5 siku tatu kabla ya siku ya Simba (Simba Day).
Kocha msaidizi wa Simba, Mrundi Masoud Djuma alisema hali ya hewa, viwanja na mahala walipofikia ni sehemu sahihi ya kufanya maandalizi ambayo wataitumia vizuri kama walivyopanga.
Djuma alisema mazingira ya hoteli waliyofikia ni nzuri, viwanja vinakizi kufanya mazoezi magumu na mepesi au programu yoyote ambayo benchi la ufundi tutakuwa tunahitaji kufanya kulingana na mahitaji yetu ya siku.
"Tupo katika mazingira yote sahihi niwapongeze viongozi kwa kuchagua eneo hili kwani linakizi mahitaji ya maandalizi ya kila timu ambayo itakuwa inataka kufanya na hiyo ndio ipo kwetu," alisema.
"Kabla ya kuondoka hapa Uturuki tutacheza mechi za kirafiki ambazo zitaonesha mwanga kuwa wapi tumeweza kupajenga na wapi kuongeza nguvu ili tukirudi nchini tuwe tupo kamili na tayari kwa kushindana kwani hata mechi ambazo tutacheza hazitakuwa na timu za kawaida," alisema Djuma.
Beki wa kati wa Simba, Paul Bukaba alisema kikosi chao kimesajiliwa wachezaji wengi na kuwa kipana zaidi ya msimu uliopita jambo ambalo litafanya kambi hiyo kuwa na hali ya kushindana zaidi.

Bukaba alisema kwanza kocha ni mpya hamfahamu kila mchezaji kama unaweza kufanya vizuri katika kambi hii ya maandalizi kila mchezaji atatengeneza uaminifu kwa mwalimu ikiwa ni pamoja na kujiandalia mazingira ya kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.
"Kama nafasi ya beki wa kati ambayo mimi nacheza tupo zaidi ya watano na kila mtu atataka kumuonyesha kocha anauwezo na anafaa kucheza katika kikosi chake cha kwanza jambo ambalo kila mchezaji anataka kulifanya hilo."
"Kiujumla tupo katika hoteli nzuri, tunatumia viwanja vizuri kufanya mazoezi na hata hali ya hewa na mazingira ya huku yanatufanya kufikilia mpira na kufanya mazoezi zaidi pengine tofauti na tungekuwa Dar es Salaam," alisema Bukaba.