Simba, Yanga zimepata darasa la kimataifa

Muktasari:

Historia nyingine imeandikwa upya katika soka la nchi yetu mwishoni mwa juma lililopita baada ya wapenzi wa soka na wananchi kwa jumla kushuhudia timu zetu vigogo wa mchezo huu hapa nchini na wakongwe kwa maana ya umri wao mkubwa tangu zimeanzishwa, wakisukumizwa nje ya mashindano makubwa ya klabu za barani Afrika

MWENZIO akinyolewa wewe tia maji, ndivyo tunavyoweza kusema Watanzania.

Historia nyingine imeandikwa upya katika soka la nchi yetu mwishoni mwa juma lililopita baada ya wapenzi wa soka na wananchi kwa jumla kushuhudia timu zetu vigogo wa mchezo huu hapa nchini na wakongwe kwa maana ya umri wao mkubwa tangu zimeanzishwa, wakisukumizwa nje ya mashindano makubwa ya klabu za barani Afrika.

Ni mwisho wa juma ambao haukuwa wa furaha kwa mashabiki na wapenda soka wengi na ni tarehe ambayo itabaki kwenye kumbukumbu zetu kwa muda mrefu.

Kwa bahati mbaya sana mechi zote mbili zilichezwa siku ya Jumamosi lakini zikitofautiana kwa saa chache. Yanga ikiwa ugenini kule Botswana katika Jiji la Gaberone ilipepetana na wenyeji wake Township Rollers kwenye mchezo wa pili wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliomalizika kwa suluhu.

Wakati hayo yakitokea, watani zao Simba walikuwa kwenye Jiji la Port Said kule Misri nao wakisubiri wakati ufike washuke dimbani dhidi ya wenyeji wao Al Masry kweye mchezo wa mkondo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika, kama wenzao nao wakatoka suluhu. Habari ya Simba na Yanga ikawa imeishia hapo.

Tofauti ni kwamba Yanga imetupwa kwenye Kombe la Shirikisho na tayari imepangiwa Weloita Ditcha ya Ethiopia kwenye mechi za mwisho za mtoano.

Msimu huu wa michezo ya Afrika ulionekana kuwa mgumu kwetu tangu mwazo licha ya timu zetu kufanikiwa kushinda hapa nyumbani kwa timu ya Simba kuichapa Gendamarie ya Djibout mabao 4-0, lakini matokeo ya mechi ya marudiano ugenini ya 1-0 yalitoa picha ya ugumu uliopo.

Pia, Yanga ilipata matokeo hafifu dhidi ya St Louis ya Shelisheli hapa nyumbani na ugenini. Dalili hii ya ugumu wa mashindano iliyojitokeza kwenye hatua ya awali iliendelea kuziandama timu hizi kongwe kwenye hatua iliyofuata.

Mara baada ya ratiba kupangwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), fununu, hofu na bahati nasibu ikaanza miongoni mwa wapenzi wa soka hapa nchini.

Kwa mawazo ya kawaida yaliyoongozwa na uzoefu, rekodi na uhalisia wa mambo katika soka la Afrika kwa sasa, kitendo cha kupangwa na Wabotswana na Wamisri hisia za mashaka zilijitokeza kwa kiwango kikubwa.

Kama hiyo haikutosha bahati mbaya michezo ya mzunguko wa kwanza ilichezwa hapa nyumbani na matokeo yakawa ni faida kwa wageni.

Kufungwa kwa Yanga mabao 2-1 katika Uwanja wa Taifa dhidi ya Township Rollers ilikuwa ni anguko kubwa lililoashiria ugumu ambao timu yetu ingekutana nayo na kukwama katika safari ya kuusaka ubingwa wa Afrika.

Kwa watani zao Simba pia mambo yalikuwa magumu baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 hapa nyumbani kila mmoja alianza kuufikiria ugumu na uzito wa kupata matokeo chanya kwenye michezo ya marudiano ugenini.

Historia imejirudia na timu zetu zikiwa zimetolewa mapema mno. Ukubwa wa kikosi cha Simba umeshindwa kuonesha faida kulingana na thamani yake.

Yanga kwa upande wake suala la kikosi chenye wachezaji majeruhi na chipukizi limekosa mashiko kwa sababu wadau wanataka timu ipate matokeo chanya. Nani wa kulaumiwa au kubebeshwa hili?

Kwa jumla timu zetu zimeshindwa kwa sababu mipango na malengo haikuwa kuishia hapa au kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrioka na kurudi kwenye Kombe la Shirikisho na mwingine kurudi kwenye ligi ya nyumbani.

Kwa miaka mingi kila tunaposhindwa hatukosi sababu zenye ladha na maana tofauti huku baadhi zikiwa ni za kimsingi na kitaalamu na nyingine hazina mwelekeo wa kiufundi.

Tumezoea pia kuelekeza lawama zetu ama kwa waamuzi, ratiba, viwanja, muda uliopangwa wa mchezo, fitina za mpira tunazokutana nazo, kukosa bahati na mengineyo.

Lakini tunajifunza nini katika mlolongo huo wa matokeo mabovu au kufanya vibaya kwa muda mrefu ili na sisi tuje na mbinu mpya kuanzia ndani ya vilabu vyetu mpaka nje na kwenye ligi zetu pamoja na kwenye michuano mikubwa ya bara zima?

Kwa vyovyote vile tunapothibitisha kwamba timu nyingi za Afrika zimepiga hatua tunatakiwa kujiuliza kwa dhati ili kutafiti kwa lengo la kujua wanachokifanya ni nini kiasi cha kutuacha tukiwa tumesimama!

Wababe wa Yanga timu ya Township Rollers iliyoanzishwa mwaka 1965 imefanikiwa kutinga hatua ya makundi kwa kishindo baada ya kuzigaragaza timu kongwe na zenye majina makubwa na historia ndefu katika soka la Afrika kama El Merreikh ya Sudan, kuna kitu cha kujifunza.

Kwa namna yoyote ile nyuma ya mafanikio haya zipo juhudi kubwa zinazohusu, mbinu za kisasa za usimamizi na uongozi wa timu, uwekezaji, usajili maridadi, uibuaji wa vipaji na kuviendeleza, utulivu ndani ya timu, matumizi sahihi ya kisasa ya rasilimali watu na fedha.

Ifike wakati timu zijitathimini upya na kwa mapana ni wapi zilipo, pamoja na uwezo wake katika kuingia kwenye soka la ushindani la kimataifa, kwa sababu kwa timu zetu za Simba na Yanga zimethibitisha pasipo shaka kwamba kama ni ubabe wa soka hapa Tanzania wao ndio wenyewe.

Kwa maendeleo na maslahi mapana ya nchi wenye dhamana ya kuzisimamia hizi klabu zipambane katika viwango vya kimataifa kwani hapa nyumbani imetosha.

Kuendelea kushangilia na kutumia nguvu nyingi kufungana zenyewe kwa zenyewe haina maana tena kwa sababu baada ya nderemo na shamra shamra za humu ndani mwisho wake ni timu zetu kurudi nyumbani vichwa chini kama yaliyowakuta safari hii na nyingine nyingi huko nyuma.

Kwa sasa huwezi kiuweka kando klabu ya Azam ambayo ni changa lakini ndiyo timu pekee hapa nchini ambayo ina sura na mwelekeo mzuri wa kisasa katika kuiendesha, ingefaa sana hata timu nyingine zikaweka nguvu kubwa kwa kuangalia mfano kutoka Azam.

Hoja inaeleweka ni uwezo mdogo wa kiuchumu, sababu ambayo haina nguvu kwa sababu uchumi ni mkakati na pia unajengwa, iwapo timu hizi zitaacha utamaduni wa kuziendesha kienyeji na kwa mazoea na badala yake zikaendeshwa kitaasisi kwa kuwaajiri wataalamu katika nyanja mbalimbali.

Tuna imani baada ya muda mfupi shida na matatizo mengi yanayosababisha zikose nguvu ya ushindani kimataifa yatapungua sana kama siyo kwisha kabisa.