Serengeti Boys kunoa makali Burundi

Wednesday April 11 2018

 

By Charles Abel

Dar es Salaam. Wakati msafara wa timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17, ukielekea Burundi leo kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati yatakayoanza keshokutwa, benchi la ufundi la timu hiyo limetamba kufanya vizuri kwenye mashindano hayo.

Mashindano hayo yanayosimamiwa na Baraza la Vyama Vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) yatafanyika kwa siku 15 kuanzia Aprili 14 hadi 28 ambapo timu mbili zitakazomaliza kwenye nafasi ya juu, zitafuzu Fainali za Afrika kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika hapa nchini mwakani.

Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Milambo alisema kikosi chake kimepata maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kwenda kufanya vizuri kwenye mashindano hayo.

"Tunataka kufanya vizuri kwenye mashindano hayo, lakini zaidi tutayatumia katika kupima ubora na ufanisi wa kikosi chetu ambacho kimekuwa kambini kwa muda mrefu. Watoto wana hamasa na molali na pia kila mmoja ana hamu ya kwenda kufanya vizuri kule Burundi," alisema Milambo.

Mkurugenzi wa timu za taifa za vijana, Kim Poulsen alisema mashindano hayo ni kipimo kwa vijana hao kuelekea Fainali za Afrika mwakani ambazo Tanzania imeshafuzu moja kwa moja kama nchi mwenyeji.

"Naweza kusema hii ni timu bora zaidi ya vijana wa umri huu ambayo nimewahi kuifundisha hapa Tanzania kwani wana vipaji vya hali ya juu ingawa kinachokosekana kwa sasa ni uzoefu tu pamoja na kupevuka kiakili. Vikipatikana hivyo nina uhakika Kombe la Mataifa ya Afrika, mwakani litabaki Tanzania.

Mashindani hayo yanafanyika kwa mara ya kwanza katika historia ya soka la ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na mechi zake zimepangwa kuchezwa kwenye viwanja vitatu vya Ngozi, Muyinga na Gitega