Serena akutana na Angelique fainali Wimbledon

Muktasari:

  • Serena anasaka taji lake la nane la mashindano hayo makubwa ya Grand Slam, likiwa taji lake la kwanza kuliwinda tangu alipojifungua mtoto wa kwanza, Septemba mwaka jana.

London, England. Bingwa mara saba wa Wimbledon kwa wanawake, Serena Williams kesho  atacheza na Mjerumani, Angelique Kerber katika fainali ya mwaka huu ya Wimbledon.
Serena anasaka taji lake la nane la mashindano hayo makubwa ya Grand Slam, likiwa taji lake la kwanza kuliwinda tangu alipojifungua mtoto wa kwanza, Septemba mwaka jana.
Nyota huyo namba moja wa zamani kwa wanawake alionyesha uwezo mkubwa alipomchapa Julia Gorges pia wa Ujerumani kwa seti mbili za 6-2 6-4, wakati Kerber naye alimshinda kwa seti mbili Jelena Ostapenko wa Latvia kwa 6-3 6-3.
Mchezo huo wa fainali utakumbushia fainali ya mwaka 2016 wawili hao walipokutana na Serena Williams kuibuka mshindi. Mwaka huo pia Serena alitwaa mataji mengine ya Grand Slam ya Australian Open na US Open.
Mbali ya kusaka taji pia katika mchezo wa kesho Serena atakua akipigania kuboresha nafasi yake ya ubora pamoja na kuandika rekodi ya kutwaa taji la 24 la Grand Slam.