Semeni sasa basi

LICHA ya timu yao kupoteza kwa penalti jana mashabiki wa Yanga walikuwa wakiwakejeli wenzao wa Simba kwamba; “Semeni sasa...” Kauli hiyo ilitokana na mabango ya Simba kabla ya mchezo huo ambao walikuwa wakitamba kwamba, Yanga angekula si chini ya mabao 3-0 hadi mapumziko.

Lakini, Simba wakawajibu na nyie semeni sasa miaka yote tukienda kwenye penalti hamtuwezi. Simba jana imethibitisha kwamba kuna MO wawili. Mmoja ni Mohammed Dewji, ambaye anawapa pesa nje ya uwanja. Mwingine ni Mohammed Ibrahim ambaye anawapa furaha ndani ya uwanja na jana Jumatano jioni alifunga penalti ya mwisho iliyoipa Simba ubingwa wa Ngao ya Hisani mbele ya Yanga.

Licha ya tambo nyingi za vigogo hao wa soka nchini, hakuna timu iliyoweza kupata bao katika dakika 90 za kawaida jambo lililopelekea kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti ambapo, Mo aliibuka shujaa kwa kuzamisha mkwaju wa mwisho.

Makipa, Aishi Manula wa Simba na Youthe Rostand wa Yanga walifanya kazi kubwa ya kupangua penalti moja kila mmoja kabla ya Juma Mahadhi kupaisha penalti iliyowapa Simba upenyo wa kushinda. Siku ilikuwa mbaya pia kwa mabeki, Kelvin Yondani wa Yanga na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambao walishuhudia penalti zao zikipanguliwa.

“Niliumia baada ya kuona Tshabalala amekosa penalti ya ushindi lakini baada ya Mahadhi (Juma) kupaisha niliona ni fursa ya kuipa Simba ushindi. Nafurahi kwamba nilifanikiwa,” alisema MO.

“Niwaambie Wanasimbahuu ni ushindi mkubwa kwao, tunawashukuru kwa kuendelea kutupa sapoti,” aliongeza.

Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisema licha ya kupoteza mchezo huo, hawajakata tamaa kwani walicheza soka safi dakika 90 ambazo hazikuwa na mbabe.

“Naweza kusema baadhi ya wachezaji wapya walikuwa na woga kidogo kwa kuwa hii ni mechi kubwa, lakini tulicheza vizuri, tulimiliki mpira na kutengeneza nafasi nyingi. Kwa kushinda kwa penalti ni kama bahati tu kwao kwani, tulicheza vizuri zaidi yao,” alisema. Wachezaji waliofunga penalti kwa upande wa Simba ni Method Mwanjali, Emanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Shiza Kichuya na MO. Wachezaji waliofunga za Yanga ni Ibrahim Ajibu, Kabamba Tshishimbi, Donald Ngoma na Thaban Kamusoko.

MCHEZO WENYEWE

Dakika 90 za mchezo wa jana zilikuwa na pilika nyingi, lakini umakini wa safu za ulinzi za kila timu ulipelekea matokeo hayo.

Simba ilionekana kucheza vizuri kwa kumiliki mpira zaidi na kutengeneza nafasi kupitia pande zote, lakini ngome ya Yanga ilikuwa imara na kuziondosha.

Laudit Mavugo na Emanuel Okwi walikosa nafasi nne za kuipa Simba ushindi huku Ibrahim Ajibu na Thaban Kamusoko wakikosa nafasi mbili ambazo pengine zingeweza kubadilisha ubao wa matokeo. Nyota wawili wa Yanga, Gadiel Michael na Kabamba ‘Tshishimbi’ ndiyo waliong’ara zaidi katika mchezo huo wakionyesha uwezo mkubwa wa kukaba na pia kupanda kusaidia mashambulizi.

TSHISHIMBI CHUPUCHUPU

Kabla ya pambano hilo la watani wa jadi jana, Simba ilikuwa ikichekea tumboni baada ya kusikia kiungo mpya wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi asingecheza, lakini mabosi wa Yanga walifanya mambo jioni na jamaa akashuka uwanjani.

Alisema mchezo wa jana baada ya mabosi wa Yanga kumnusuru dakika za jioni kufuatia vikwazo vilivyokuwa vimewekwa na klabu yake ya Mbabane Swallows ya Swaziland iliyokuwa inataka ilipwe chake kwanza.

Mbabane ilikuwa inataka ilipwe Dola 30,000 ili kufuta machungu ya kuzikosa dola 70,000 zilizoletwa na Orland Pirates ya Afrika Kusini iliyokuwa ikimtaka, lakini mabosi wa Yanga walikuwa tayari kutoa fedha pungufu na kugomewa. Ndipo mabosi wa Yanga wakapiga harambee na fasta zikapatikana kiasi cha fedha zilizotakiwa na Mbababe kulipwa na kuiachia ITC ilimruhusu kiungo huyo kucheza.

SIMA AONJA JOTO

Katibu Mkuu wa Singida United, Abdulrahman Sima, jana alionja kadhia ya mechi kubwa baada ya kuzuiwa na mmoja wa walinzi kwa muda mlangoni wakati akitaka kwenda Jukwaa Kuu la Uwanja wa Taifa kwa mdai ya kutotambulika.

Sima aliyefika uwanjani hapo akiwa na msaidizi wa ofisi yake, licha ya kufanikiwa kuingia ndani ya geti kubwa la uwanja huo, alikutana na kigingi cha mmoja wa walinzi kuingia jukwaa la watu maalum (VIP) lililotengwa kwa ajili ya viongozi mbalimbali wakiwemo wa klabu za soka zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hata hivyo, baadaye aliruhusiwa kuingia baada ya mlinzi huyo kujiridhisha kutoka mmoja wa maofisa wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kwenda kuketi katika eneo hilo lililoandaliwa kwa ajili yao.

JEZI MPYA SIMBA

Simba bwana inapiga pesa bwana, kwani jezi zao mpya zenye nembo ya SportPesa jana ziligeuka bidhaa adimu kwa kugombewa kwa wingi na mashabiki wa klabu hiyo hali iliyofanya zimalizike mapema kwa wafanyabiashara waliokuwa wakiziuza nje ya Uwanja wa Taifa.

Hadi kufika saa 7 mchana, jezi hizo ambazo zimetambulishwa wiki tatu zilizopita katika tamasha la Simba Day, zilikauka kwa wafanyabiashara hao ambao hutundika jezi zao kwenye miti iliyopo pembezoni mwa barabara inayopita uwanja huo jambo, lililofanya waanze kuhaha kusaka nyingine za kuuza.

Rajabu Ramadhan, mmoja wa wafanyabiasha wanaouza jezi na bidhaa nyingine kwa mashabiki, aliliambia gazeti hili kuwa biashara ya jezi hizo imeenda vizuri kutokana na mashabiki wa Simba kukoshwa na usajili uliofanywa msimu huu.

WALANGUZI WABANWA

Pambano la jana la watani lilikuwa na mkosi kwa walanguzi wa tiketi waliokuwa na tabia ya kupandisha bei ya tiketi za kuingilia Uwanja wa Taifa kutazama mechi, baada ya kampuni ya Selcom kuwaba kimtindo.Tofauti na hapo awali ambapo kampuni hiyo iliweka watu wa kuuza kadi pamoja na tiketi za kuingilia uwanjani kwenye maeneo mbalimbali yanayozunguka uwanja huo, jana ilikuja na utaratibu wa mawakala wake kuuza kadi na tiketi wakiwa ndani ya uzio wa Uwanja wa Taifa na ule wa Uhuru jijini.