Sanchi kumbe wala sio mchina babaake

ASIKUAMBIE mtu, humu duniani kuna watu wameumbwa bwana. Bahati nzuri Tanzania ni miongoni mwa waliojaliwa kuwa na wasichana warembo. Mmoja ya wadada wanaotikisa kwa sura na umbile la kuvutia ni Sanchi. Ndio, mashabiki wake wanamjua zaidi kwa jina hilo, japo wazazi wake walimpa jina la Jane Ramoy.

Sanchi ni mwanamitindo wa kimataifa na mjasiriamali anayetamba nchini na Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Mwanadada huyo amejaliwa figa matata na kwa bahati nzuri, Mwanaspoti limefanikiwa kufanya naye mahojiano maalum ambapo Sanchi amejiachia kwa raha zake akiweka bayana maisha yake na mambo ambayo mashabiki wake hawakuwa wakiyajua. Endelea naye...!

Mwanaspoti: Mambo vipi Sanchi?

Sanchi: Poa, naongea na nani?

Mwanaspoti: Unaongea na Mwanaspoti hapa.

Sanchi: Ok, unasemaje?

Mwanaspoti: Nilikuwa nahitaji kuonana na wewe kwa ajili ya mahojiano, kuhusu shughuli zako za Uanamitindo na maisha yako nje ya kazi zako.

Sanchi: Duu! Sawa ila kuonana itakuwa ngumu maana niko mbali, labda tufanye mahojiano kwenye simu.

Mwanaspoti: Hivi unashughulika na nini haswa, maana kuna wakati unakuwa kimya sana?

Sanchi: Mimi ni Mwanamitindo na mfanyabiashara wa nguo na urembo.Pia biashara zangu huchanganyachanganya kwa asilimia kubwa na dili na urembo wa kina dada.

Mwanaspoti: Kwanini unapenda kupiga picha zinazo kuacha nusu utupu?

Sanchi: Ni hobi yangu tu, najisikia furaha kufanya hivyo kwa sababu niko huru na kazi zangu.

Mwanaspoti: Kuna tetesi unaendesha maisha kwa kutegemea umbo lako, ni kweli?

Sanchi: Hakuna maisha yanayoendeshwa hivyo, hivi ukiwa na umbo tu, kwani watu wasiokuwa na maumbo maisha yao yanaendaje?

Mwanaspoti: Kuna habari unapenda kujirahisisha kwa mapedezee wa mjini kwa kutumia umbo lako kwa kulinadi ili upate pesa, je ni kweli?

Sanchi: Sio kweli, sijawahi na siwezi kupoteza thamani ya umbo langu kwa sababu ya pesa. Kwanza siku hizo hakuna mapedezee bwana.

Mwanaspoti: Umeolewa na una watoto wangapi?

Sanchi: Hapana bado sijaolewa na wala sina mtoto, ila nina mpango wa kuzaa mwakani tukijaliwa. Tuombe Mungu tufike salama. Nami napenda kuitwa mama.

Mwanaspoti: Kuna madai kuwa, wanaume kwa sasa wanaogopa kukuoa tangu ulipotangaza kuwa mahari yako si chini ya Sh10, hili nalo unaliozungumzaje?

Sanchi: Haahaahaa, ukiona hivyo hao sio waoaji na kama kweli wanaogopa basi itanisaidia kupata mwanaume sahihi wa maisha yangu pale atakayetokea kunioa kwa mahari hiyo.

Mwanaspoti: Kutokana na umbo lako ni usumbufu gani unaopata?

Sanchi: Kwanza nikitembea barabarani huwa baadhi ya wanaume wananiudhi sana kwa jinsi wanavyonipigia kelele za miluzi na katika simu yangu kila siku namba mpya zinapigwa na ukipokea utasikia mtu anakwambia ananipenda. Hapo humjui na hujui namba yangu kaipata wapi. Ndio maana mara nyingi napenda kukaa ndani siku nzima tu hata siku tatu kwa ajili ya kukwepa usumbufu huo.

Mwanaspoti: Je ni kweli eti unatumia dawa za kichina ili kukuza makalio yako?

Sanchi: Hapana aisee, siwezi kufanya upuuzi huo, hili ni umbo langu halisi la kuzaliwa. Ni kweli watu wengi wamekuwa wakisema hivyo, ila kwanini mitumie dawa za kichina na kwa kutaka nini jamani?

Mwanaspoti: Tupe historia yako kwa ufupi?

Sanchi: Kwa kifupi, nimezaliwa June 24, Mkoa wa Kilimanjaro. Ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wa tatu. Kielimu nina shahada ya masuala ya Fedha na Benki.