Rostand aishika pabaya Yanga

Muktasari:

Yanga ilitangaza kuvunja mkataba na Rostand kutokana na kutoridhishwa na kiwango chake na kuelezwa ingemlipa miezi minne iliyosalia ya mkataka wake akiwa Jangwani. Kipa huyo Mcameroon alikuwa akilipwa Dola 1,200 (sasa na Sh2.7 milioni).

ALIYEKUWA kipa wa Yanga, Youthe Rostand ameishika pabaya klabu hiyo baada ya kuweka wazi mipango yake ya kuiburuza Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) iwapo mabosi wake wa zamani watashindwa kumlipa fedha kama walivyokubaliana wakati wa kuvunja mkataba wake.

Yanga ilitangaza kuvunja mkataba na Rostand kutokana na kutoridhishwa na kiwango chake na kuelezwa ingemlipa miezi minne iliyosalia ya mkataka wake akiwa Jangwani. Kipa huyo Mcameroon alikuwa akilipwa Dola 1,200 (sasa na Sh2.7 milioni).

Rostand alivunjiwa mkataba na Yanga baada ya kuonekana kiwango chake kushuka, licha ya mchezaji huyo kubakiza mkataba wa mwaka mmoja wa kukipiga na wanajangwani hao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Rostand alisema licha ya kwamba hayupo ndani ya Yanga, anajua sehemu gani ambayo atapata haki zake za msingi ambazo zimesalia ndani ya kikosi hicho baada ya kuvunjiwa mkataba wake.

“Ukienda TFF utakuta barua yangu ambayo niliipeleka, nasubiri kwanza kuona kama nitapata haki zangu, lakini ikishindikana hapo basi itabidi niende juu zaidi (Fifa), kwa vyovyote vile haki yangu italipwa tu kwa kufuata mkataba unavyosema.”