Roma yajitosa kwa Riyad Mahrez

Friday July 21 2017

 

Roma, Italia. Miamba ya Serie A, Roma ipo tayari kumsajili nyota Algeria, Riyad Mahrez kutoka Leicester City, kwa mujibu wa Sky, Italia.

Mahrez amekuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha Leicester tangu alipojiunga na Le Havre mwaka 2014 na kuisaidia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 2015/16, na kufanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa PFA.

Pia, kiungo huyo ameisaidia Leicester kufuzu kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa UEFA msimu uliopita.

Hata hivyo, mwezi Mei aliomba kuondoka ndani ya Uwanja wa King Power, wakati akihusishwa na kutakiwa na Barcelona na Arsenal.

Kocha wa Leicester, Craig Shakespeare aliimbia Sky Sports wiki iliyopita kuwa hajapokea ofa yoyote ya Mahrez, lakini ujio wa Roma unafungua upya mjadala huo.

Klabu hiyo ya Italia inamtazama nyota huyo wa Algeria kama ndiye mrithi sahihi wa Mohamed Salah, waliyemuuza kwa Liverpool mwezi uliopita.