Rekodi zainyima ushindi Simba SC

Muktasari:

Simba ilianza kwa ushindi mnono dhidi ya Ruvu Shooting ilipofunga mabao 7-0, ikatoka sare ya 1-1 na Azam FC, ikaishinda Mwadaui 3-0, ikatoka sare ya 2-2 na Mbao FC, ikaishinda Stand United 2-1, ikatoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar.

TANGU msimu huu wa Ligi Kuu Bara uanze, Simba imekuwa na rekodi ya kushinda mechi moja na kutoa sare inayofuatia, jambo linaloweza kuinyima ushindi dhidi ya Prisons zitakapoumana Novemba 18 katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Simba ilianza kwa ushindi mnono dhidi ya Ruvu Shooting ilipofunga mabao 7-0, ikatoka sare ya 1-1 na Azam FC, ikaishinda Mwadaui 3-0, ikatoka sare ya 2-2 na Mbao FC, ikaishinda Stand United 2-1, ikatoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar.

Kisha ikashinda mabao 4-0 dhidi ya Njombe Mji, ikaja mechi ya watani na kutoka 1-1 na Yanga kisha wakaishinda Mbeya City bao 1-0.

Kufuatia rekodi hiyo, Simba inayoongoza kwa pointi 19 sawa na Azam, itakuwa na kibarua kigumu cha kuishinda Prisons.

Hata hivyo, Simba haina rekodi ya kuvuna pointi sita mkoani Mbeya, mara nyingi wakiishinda City, wanafungwa na Prisons.

Kocha wa zamani Polisi Moro na Kagera Sugar, Adolf Rishard, amesema: “Kwanza ninaweza kusema umakini wa maandalizi hupungua, wanajisahau wanaposhinda mechi, wanaona wamemalizika kila kitu, lakini kwa namna nyingine, walizotoka sare ni kipimo cha uwezo wao.”

Rishard alisema tayari wamepoteza pointi nane kwa sare nne ambazo wametoka, jambo alilosema si zuri kwa klabu yao inayowania ubingwa wa ligi kuu.

Nyota wa zamani wa Mecco ya Mbeya, Abeid Kasabalala, alisema ili waweze kuishinda Prisons, wachezaji waione rekodi hiyo itawapotezea malengo.