Polisi FC wanyakuwa kibabe ng’ombe Mapesa Cup

Muktasari:

  • Hatua hiyo imefanya timu ya Mageta kutema ubingwa huo kwani msimu uliopita waliweza kutwaa Taji hilo na sasa wamewakabidhi maafande hao.

SERENGETI. KAMA zali mwanangu, Maafande wa Polisi FC wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapesa baada ya kuwafunga Mageta Stars kwa mikwaju ya penalti ya 4-3.
Hatua hiyo imefanya timu ya Mageta kutema ubingwa huo kwani msimu uliopita waliweza kutwaa Taji hilo na sasa wamewakabidhi maafande hao.
Katika mtanange huo ndani ya dakika 90 uliopigwa Uwanja wa Sokoine mjini hapa  timu hizo zilitoka Suluhu jambo lililofanya zipigwe penalti hizo.
Kwenye mikwaju hiyo ya penalti timu ya Polisi iliweza kufunga Nne huku wapinzani wao wakipata tatu ambapo kipa wa Maafande hao Casmir Charles aliweza kuokoa mbili.
Kocha wa Polisi,Sharifu Kibaye aliwapongeza wachezaji wake kwa kuweza kunyakuwa taji hilo ambapo amesema kazi haikuwa rahisi kutokana na upinzani wa timu zilizoshiriki Ligi hiyo.
Kwa ushindi huo Polisi waliweza kujinyakulia Ng’ombe Mmoja pamoja na Seti ya jezi, mpira na kikombe huku Mageta wakipata Ng’ombe mmoja na mpira.
Mshindi wa tatu ambaye ni timu ya Seronga waliambulia mbuzi wawili na mpira mmoja huku Mfungaji Bora,  Martine Remijusi aliyefunga mabao 10 wakipata Sh20,000.