Pochettino hali tete Spurs !

Muktasari:

Hata hivyo baada ya timu kufungwa mabao 2-1, na Inter Milan ya Italia katika mechi ya kwanza kundi B, Ligi ya Mabingwa Ulaya, alibadilika na kusema timu ilicheza vizuri ila ilikosa bahati.

London, England. Ingawa mashabiki wa Tottenham wanasifika kwa utulivu miongoni mwa mashabiki wa timu za England, lakini safari hii uvumilivu umewashinda na wamemjia juu kocha wa timu hiyo, Mauricio Pochettino.

Hicho kilikuwa kipigo cha tatu kwa Spurs msimu huu, walifungwa mabao 2 -1, na Liverpool na Watford katika mechi za Ligi Kuu England vipigo vilivyoirudisha nyuma iliyochezwa Vicarage Road.

Mashabiki hao walikerwa na majibu ya Kocha huyo aliyewaambia yeye ndiye mwenye uamuzi wa mwisho wa kikosi chake, akiwaambia aulizwe tu kama timu itafungwa lakini si nani atacheza na nani akae benchi.

Pochettino alionyesha kujistukia baada ya waandishi kumuuliza iwapo anadhani kuwaacha walinzi wake mahiri, Toby Alderweireld na Kieran Trippier kumeigharimu timu, alikataa kujibu swali hilo.

Kilichowakera mashabiki hao ni uamuzi wa Pochettino kuamua kuwaacha walinzi mahiri wa timu hiyo Toby Alderweireld raia wa Ubelgiji na Mwingereza, Kieran Trippier, katika safari ya kwenda San Siro kwa hoja dhaifu ya kuwapumzisha.

Mbali ya wachezaji hao Pochettino, pia aliwaacha kipa namba moja Hugo Lloris na washambuliaji  Dele Alli na Moussa Sissoko ambao ni majeruhi.

Akijibu hilo alisema kwa mara ya kwanza msimu huu timu yake ilicheza vizuri na anaamini bahati haikuwa upande wao, kwani ilipata bao la kuongoza lililofungwa na Christian Eriksen dakika ya 53 na wenyeji walisawazisha na kupata ushindi dakika tano za mwisho.

“Nadhani tumecheza vizuri kuliko mchezo wowote wa msimu huu, naamini kuanzia sasa timu itarejea kwenye wimbi la ushindi, natamani mashabiki waendelee kutuunga mkono,” alitamba Pochettino.