Kocha Man City aanza kuchonga

Muktasari:

Man City imeweka rekodi ya kushinda mechi 15 kati ya 16 za Ligi Kuu England msimu huu  

MANCHESTER, ENGLAND.Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amempiga kijembe mtani wake Jose Mourinho kwa kumwambia timu yake ya Manchester United si Chelsea wala Tottenham Hotspur zinazocheza mpira unaoeleweka.

Kauli hiyo ya Guardiola ni ishara kwamba hana wasiwasi na Mourinho kwa sababu Man United yake haina uwezo wa kumkamata.

Man United na Man City kwa sasa zimetofautiana pointi 11 na wachambuzi wa masuala ya soka wanaamini vita iliyobaki kwenye ligi hiyo kwa sasa ni ya kuwania Top Four kwani ubingwa tayari umeshafahamika unakwenda Man City.

Hata hivyo, Mourinho hataki kuamini hilo, akisema kama ubingwa wa ligi ungekuwa na mwenyewe kwa sasa basi angekuwa amekwenda zake likizo huko Brazil au Marekani.

"Tottenham na Chelsea ni timu bora kutokana na namna zinavyocheza soka lao. Hawaangalii mpinzani anachezaje, wao wanacheza soka lao. Huo ndiyo mtihani kwetu," alisema Guardiola.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Guardiola inadaiwa kama ni ujanja tu wa kutaka kuwapumbaza Spurs ambao atakumbana nao leo Jumamosi huko Etihad.

Kama Man City itashinda mechi hiyo basi wataweka pengo la pointi 14 dhidi ya Man United, ambao wao watasubiri hadi kesho Jumapili kucheza na West Brom kwao.

Makocha ambao wameonekana kukata tamaa kuhusu ubingwa ni Jurgen Klopp wa Liverpool na Antonio Conte wa Chelsea, licha ya baadhi ya mastaa wake kuamini kwamba bado wapo kwenye vita hiyo ya kuikimbiza Man City kileleni.

Kocha Arsene Wenger wa Arsenal anaungana na Mourinho wanaoamini kwamba kuna sehemu tu Man City watakwama kama si sasa basi hata baadaye, hivyo ubingwa wa ligi hiyo basi kinachowezekana kubebwa na yeyote licha ya pengo hilo la pointi lililopo kwa sasa.

Guardiola kwa upande wake amekuwa na wasiwasi pia akiwaonya wachezaji wake kwamba kushinda mechi 15 mfululizo kwenye Ligi Kuu England hakitakuwa kitu cha maana kama watakosa ubingwa wa ligi hiyo, huku ushidani unadaiwa utakuwa mkali zaidi kuanzia sasa hadi kwenye kuukamata Mwaka Mpya.

Guardiola na Man City yake atakuwa na shughuli dhidi ya Spurs, ambao kwa miaka ya karibuni wamekuwa wakivuna matokeo mazuri kila wanapocheza na wababe hao wa Etihad.

Mechi nyingine za ligi hiyo, Leicester City wao watakuwa na shughuli dhidi ya Crystal Palace, wakati vijana a Conte, Chelsea watakuwa Stamford Bridge kuwakaribisha Southampton, huku Watford wakicheza na Huddersfield.

 Brighton wataonyeshana kazi na Burnley, wakati Stoke City watakuwa na kasheshe mbele ya West Ham na Arsenal wanajipumzisha kwao Emirates kumkaribisha Rafa Benitez na kikosi chake cha Newcastle United.

 Kesho kutapigwa mechi nyingine Bournemouth na Liverpool, huku Everton wakisubiri hadi Jumatatu kucheza na Swansea City.