Panga la Masoud lamsubiri MO tu

Muktasari:

Kwa wiki kadhaa sasa kuna taarifa kwamba Kocha Masoud yupo mbioni kutimuliwa kikosini kwa kile kilichoelezwa kutoelewana na bosi wake na juu ya tuhuma za utovu wa nidhamu, lakini mabosi wa Msimbazi wanajifanya kukausha.

INGAWA mabosi wa Simba wamekuwa wasiri sana juu ya kile kinachoendelea baina ya Kocha Mkuu wao Patrick Aussems na Msaidizi wake, Masoud Djuma, lakini siri zimevuja kuwa, siku za Mrundi Msimbazi zinahesabika tu kwa sasa.

Kwa wiki kadhaa sasa kuna taarifa kwamba Kocha Masoud yupo mbioni kutimuliwa kikosini kwa kile kilichoelezwa kutoelewana na bosi wake na juu ya tuhuma za utovu wa nidhamu, lakini mabosi wa Msimbazi wanajifanya kukausha.

Hata hivyo imebainika, hatma ya Masoud inamsubiri Bilionea Mohammed ‘Mo’ Dewji ambaye kwa sasa yupo safari ili aje kutoa baraka za kocha huyo kusepa.

Masoud hajaambatana na Simba kwenda Mtwara kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa jioni ya jana, akitakiwa kubaki na wachezaji 10 walioachwa Dar.

Baada ya kuachwa kwa kocha huyo kumekuwepo na sintofahamu kwa wadau wa soka nchini huku wengine wakidai kuwa kitendo hicho hakijakaa sawa.

Imeelezwa kwamba baada ya kuwepo kwa madai hayo uongozi wa Simba ulikaa kikao na Masoud ambapo sasa anaishi kwa uangalizi, huku ikidaiwa kuna maamuzi magumu yanaweza kufanywa muda wowote kuanzia wiki ijayo.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema mabosi wa Simba wanaendesha kwa sasa vikao vyao kama Bodi ya Wakurugenzi watakutana chini ya Mo Dewji ili kujadili hatma ya Masoud, ingawa chanzo hicho kinasema Mrundi ana asilimia chache za kubaki Msimbazi.

Masoud ameajiriwa Simba msimu uliopita akiwa msaidizi wa Joseph Omog raia wa Cameroon ambaye pia alifungashiwa virago, huku Mrundi huyo akichukua nafasi ya Mganda Jackson Mayanja.

“Nafasi ya Masoud (Djuma) ni ndogo sana, Mo kwa sasa amesafiri, ndiye pekee anayesubiriwa maana kikao cha pamoja naye ndicho kitaamua hatima ya kocha huyo kubaki ama kuondolewa, ila asilimia za kubaki ni chache sana, unajua ni vigumu kufanyakazi kwenye benchi la ufundi kukiwa hakuna maelewano.

“Hayo si malalamiko ya kwanza kwa Aussems, hivyo muda sio mrefu lolote linaweza kutokea kwa Masoud na kama ataondoka Aussems atasaidiana na kocha wa viungo Adel Zrane,” alisema kiongozi huyo aliyeomba kuhifadhiwa jina.

MSIKIE TRY AGAIN

Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alifafanua juu ya hilo kwamba; “Kutofautiana kati ya mtu na mtu ni jambo la kawaida, watu wanatofautiana lakini wanayamaliza ili maisha yaendelee, Masoud amebaki Dar es Salaam kwa sababu maalumu ambazo ni kuwasimamia wachezaji 10 waliobaki.

“Wachezaji waliobaki wote wanaweza kutumika kwenye kikosi cha Simba, hivyo ni lazima waendelee na ratiba nyingine ndio maana hatukusafirisha wachezaji wote tuliowasajili ambao hawatacheza kwani ingekuwa gharama zaidi na mtu sahihi wa kubaki nao ni Masoud.

“Unajua hivi sasa kila mtu atazungumza anavyojisikia, ila ukweli hakuna mambo kama hayo kwamba amesimamishwa wala kuondolewa kikosini, Masoud bado ni mwajiriwa wetu, vikao ndani ya Simba hukaa kila siku, hivyo sidhani kama kuna kikao maalumu kwa ajili ya hilo,” alisema Try Again.

MASOUD HUYU HAPA

Juzi Ijumaa, Kocha Masoud alikuwepo Uwanja wa Uhuru kuzishuhudia African Lyon na Coastal Union ya Tanga zikicheza katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu lakini mwonekano wake ulizua maswali kwa mashabiki waliohudhulia uwanjani. Kocha huyo alionekana kuwa kwenye dimbwi la mawazo, japo hakuacha kufanya kile kilichompeleka uwanjani hapo kwa kuandika kila kilichokuwa kinaendelea uwanjani.

Mwanaspoti lilizungumza naye baada ya gemu hilo akasema, “Siwezi kuzungumzia chochote kwani nitakuwa natoa siri, udhaifu wao.”

Kuhusu hatma yake alisema: “ Kama kuna jambo lolote linakuja mbele langu nitalipokea, iwe kubaki ama kuondoka, nikiondoka nitawaaga kama nilivyokaribishwa kwani sijaua, nitarejea kwetu na hivyo sina hofu na jambo lolote litakalotokea mbele yangu.”