Uzoefu wa Okwi, Niyonzima wampa presha Kichuya

Thursday October 12 2017

 

By OLIPA ASSA

WINGA machachari wa Simba, Shiza Kichuya amefichua kuwa uwepo wa Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima katika klabu hiyo umemgusa kwa namna moja ama nyingine na kubadilisha mtazamo wake kwa namna alivyokuwa akichukulia mambo.

Ameeleza kuwa mastaa hao wana kiwango cha kimataifa kutokana na uzoefu wao na walikopitia jambo ambalo linampa changamoto ya kutathimini kazi yake ili ajue kitu gani anatakiwa kukiboresha.

"Ndani ya mechi tano ambazo tayari tumecheza nimejifunza vitu vingi hasa kwa mastaa hao. Kwanza uzoefu wao unawabeba, wanajua kitu cha kufanya kwa kila mechi, hilo linafanya mazoezi yangu yawe zaidi kuliko wao," alisema.

"Mimi nimetoka Mtibwa Sugar, na kujiunga na Simba, lakini wao wamepitia klabu tofauti zenye ujuzi tofauti, naamini nikitulia na kujua siri iliyowafanya wafike hapo, nitafika mbali zaidi kuliko kujifanya mjuaji," alisema.