Nyota Singida waitamani Yanga

Wednesday January 10 2018

 

By THOBIAS SEBASTIAN, UNGUJA

NYOTA wa zamani wa Yanga, Ally Mustapha, Kiggi Makassi na Nizar Khalfan ambao wanacheza katika kikosi cha Singida United wanatamani kupata matokeo ya ushindi katika nusu fainali yao ya leo na Yanga nao washinde ili wakutane  hatua ya fainali ya Kombe la Mapinduzi.

Timu hizo zimekutana hatua ya makundi mechi ya mwisho na kumaliza kwa sare ya kufungana bao 1-1,  Danny Lyanga alifunga kwa Singida na Said Juma kwa Yanga wakamalizika na pointi 10, kila mmoja.

“Yanga tulikutana nao katika ligi tukatoka sare na tulivyokutana huku tulitamani kuona tunawafunga kwani hata kocha alikuwa anataka kuona hivyo lakini yote kwa yote mechi ikamalizika kwa sare,” anasema Makassi.

“Tunaomba Mungu atujalie tushinde mechi ya nusu fainali na Yanga kwao iwe hivyo ili tukutane tena katika hatua ya fainali kwani hatutafanya tena makosa ambayo tuliyafanya kwenye mechi mbili zilizopita.”

Barthez anasema, Yanga walisawazisha dakika za mwishoni baada ya kupoteza umakini, wao walifikiri wameshashinda kumbe mechi ilikuwa bado.

“Tulipoteza tu umakini Yanga wakasawazisha lakini kama tutakutana nao tena hatutafanya uzembe kama huo zaidi ya kuzidisha umakini ili kupata ushindi dhidi yao,” anasema Barthez ambaye msimu uliopita alikuwa na kikosi cha Yanga.

Kocha wa Singida, Hans Pluijm anasema mechi za Yanga zote ni zakawaida kwao ila wanajipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri dhidi yao kila wanapokutana nao.

“Yanga ni timu nzuri na kubwa lakini tumekutana kaatika mashindano haya tukiwa na ratiba ngumu ya kucheza mara kwa maara na hata matokeo yaliyotokea ni kutokana na kucheza mfululizo,” anaeleza Pluijm.