Njombe Mji ipo tayari kuikabili Prisons

Mbeya. Timu ya Njombe Mji itakayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza  msimu huu imeanza kucheza mechi za kirafiki ikijiandaa na mechi yake ya kwanza ligi hiyo dhidi ya  Tanzania Prisons.

Njombe Mji itafungua pazia la Ligi Kuu Agosti 26, ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Sabasaba dhidi ya Prisons iliyojichimbia Zanzibar.

Timu hiyo iliyorejea Njombe juzi ikitoka Mkoani Ruvuma ilikokwenda kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya JKT  Mlale ya daraja la kwanza na kuifunga mabao 2-0 pamoja na Majimaji FC  iliyotoka sare ya bao 1-1.

Msemaji wa klabu hiyo, Solanus Mhagama alisema baada ya timu kurejea mkoani hapo itaendelea na mazoezi yake ya kawaida.

Alisema timu hiyo itaendelea kujinoa katika Uwanja wa Sabasaba na hawana hofu na Prisons walishawahi kucheza nao kwenye mashindano ya ujirani mwema iliyokuwa ikifanyika wilayani Kyela mkoani hapa.

Mhagama alisema wamecheza mechi nyingi anaimani mehi hizo zikatakuwa zimetoa mwanga kwa kocha mkuu Hassan Banyai pamoja na kocha  msaidizi Mrage Kabange  kujua kikosi chao.