Niyonzima anasubiri ruksa

Muktasari:

  • Niyonzima alisema kwa sasa anajihisi yupo fiti baada ya matibabu yake nchini India, lakini hawezi kufanya lolote mpaka ruksa maalum ya daktari ili aungane na wenzake waliorejea alfajiri ya leo wakitokea Misri walipoenda kucheza na Al Misry.

KIUNGO fundi wa Simba, Haruna Niyonzima anaendelea vizuri, ila anasubiri ruksa tu kutoka kwa daktari wa timu hiyo Yassin Gembe ili kuanza kujifua na wenzake labla ya kuliamsha upya katika Ligi Kuu Bara.

Niyonzima alisema kwa sasa anajihisi yupo fiti baada ya matibabu yake nchini India, lakini hawezi kufanya lolote mpaka ruksa maalum ya daktari ili aungane na wenzake waliorejea alfajiri ya leo wakitokea Misri walipoenda kucheza na Al Misry.

“Najiona ninaendelea vizuri, nipo tayari kuitumikia timu, lakini madaktari wangu ndio wenye maamuzi ya mwisho kuwa wataniruhusu nianze kufanya mazoezi na wenzangu au niendelee kufanya mazoezi yangu binafsi,” alisema Niyonzima.

“Ninahamu kubwa ya kurudi uwanjani na kuhakikisha naisaidia timu kufikia malengo tuliyojiwekea msimu huu, natamaani kuanza kazi chini ya Pierre Lechantre ambaye tangu aje Simba nilikuwa majeruhi,” alisema Niyonzima.

Kiungo huyo kutoka Rwanda, alisajiliwa Simba msimu huu akitokea Yanga akiwa kama kabadilishana na Ibrahim Ajibu aliyetoka Msimbazi na kutua Jangwani.