Ninje awapa tahadhari wachezaji Kili Stars

Muktasari:

Ninje ambaye aliwaita wachezaji 20 kuunda kikosi hicho kinachotarajiwa kuingia kambini Novemba 26 kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Chalenji inayotarajiwa kuanza Desemba 2 nchini Kenya.

KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania Bara, ‘Kilimanjaro Stars’, Ammy Conrad Ninje amesema, aina ya wachezaji anawaowahitaji ndani ya kikosi chake ni wale wanaotaka kufundishwa na wanaofundishika.
Ninje ambaye aliwaita wachezaji 20 kuunda kikosi hicho kinachotarajiwa kuingia kambini Novemba 26 kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Chalenji inayotarajiwa kuanza Desemba 2 nchini Kenya.
“Kwanza nataka mchezaji ambaye ana njaa ya mafanikio, atambue sehemu pekee ya kupata mafanikio  ni kucheza timu ya taifa, nataka wachezaji wanaofundishika na wanaokubali kufundishika,” alisema Ninje ambaye ni kocha wa Daraja ‘A’ la Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA).
Wachezaji wanaotarajiwa kuingia kambini Jumapili ya Novemba 26, mwaka huu jijini Dar es Salaam ni pamoja na makipa, Aishi Manula (Simba SC) na Peter Manyika (Singida United).
Walinzi ni Gadiel Michael (Young Africans), Boniphace Maganga (Mbao FC), Kelvin Yondani (Young Africans), Kennedy Juma (Singida United), Erasto Nyoni (Simba SC) na Mohammed Hussein (Simba SC).
Viungo wa kati ni Himid Mao ambaye ni Nahodha (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Mzamiru Yassin (Simba SC), Raphael Daud (Young Africans), Shizza Kichuya (Simba SC), Abdul Hilal (Tusker/Kenya) na Ibrahim Ajib (Young Africans).
Washambuliaji ni Mbaraka Yussuph (Azam FC), Elias Maguri (Dhofar/Mascat, Oman), Daniel Lyanga (Fanja FC/Mascat) na Yohana Mkomola (Ngorongoro Heroes).
Benchi la Ufundi linaundwa na yeye Ninje ambaye ni Kocha Mkuu, Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa).
Katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Desemba 3, mwaka huu, Kilimanjaro Stars imepangwa Kundi ‘A’ pamoja wenyeji Kenya, Rwanda na Libya ambayo ni timu mwalikwa kutoka Kaskazini mwa Afrika.
Kilimanjaro Stars ambayo imewahi kutwaa mara tatu taji hilo la Chalenji tangu kuanzishwa kwake, itaaza kampeni za kurudisha heshima yake dhidi ya Libya katika kundi hilo la A utaofanyika Desemba 3, mwaka huu.