Neema yatua vibanda umiza, wazee wa mikeka Kombe la Dunia

Wednesday June 13 2018

 

By ELIYA SOLOMON NA OLIPA ASSA

VIBANDA umiza, mabaa na sehemu mbalimbali, mishare ya saa 12:00 jioni kesho Alhamisi vitakuwa na nyomi ya watu, kuwatazama wenyeji wa Kombe la Dunia Urusi na Saudi  Arabia, kwenye nyasi za Uwanja wa  Luzhniki mjini Moscow.
Bila kuwasahau wazee wa mikeka kupanga foleni ama simu zao kujaza mabando kwa ajili ya kujaribu bahati zao za kubashiri nani anashinda katika muendelezo wa Kombe hilo.
Mambo yanaanza kesho kwa ufunguzi ambao utapambwa na  sherehe za maonyesho mbalimbali ya sanaa  na miongoni mwa washereheshaji  wanaotajwa ni mikali wa muziki wa  Rock  nchini England, Robbie Williams.
Pia  msanii , Nicky Jam ambaye yupo chini ya rekodi lebo ya RCA nchini Marekani  atatumbuiza ngoma rasmi kwenye mashindano hayo, iitwayo Live it Up akishirikiana na wakali wengine kama muigizaji,  Will Smith na  Era Istrefi.
Ngoma hiyo, imebeba ujumbe mzito wa kuwaweka watu  pamoja kwa ajili ya kombe hilo la Dunia japo Jason Derulo na Diamond Platnumz nao wanatajwa kwa upande wa Coca- Cola kuhusika na ushereheshaji huo.
Awali ni Derulo pekee ambaye alitengeneza ngoma rasmi ya kombe la Dunia kwa upande wa kampuni ya Coca Cola iitwayo, Colours kwa maana ya rangi za bendera za mataifa mbalimbali kwa lengo la kuwa pamoja kuelekea kwenye mashindano hayo.
Lakini mkali huyo wa Marekani  ambapo ndio wanatamba kimuziki duniani, amefanya kwa mara ya pili ngoma hiyo yenye ladha ya lugha tofauti, ikiwemo na Kiswahili.
Mwanaspoti inakuletea ngoma tano  tofauti za Kombe la Dunia ambazo zilibamba kila kona katika ufunguzi na michuano hiyo mikubwa zaidi duniani.
Santana - We Will Find a Way (2014)
Carlos Santana ni Mexico ambaye alijipatia umaarufu kwenye miaka ya  1960 na 1970, msanii huyo akishirikiana na  Wyclef Jean,  Avicii na  Alexandre Pires waliisuka We will find a way iliyokuwa inazungumzia njia iliyokuwa inaenda kutafutwa.
Kwenye wimbo huo, kuna kipande kinasema pale ambapo unakosa chakula, unapopoteza usingizi, unapohangaika mtaani huwezi kuficha mapenzi ya moyo wako.
Tunaungana wote kwa pamoja japo tunatofautiana rangi ya bendera zetu…Kilitumbuizwa vyema hicho kibao kilichonakishiwa na Kireno kwa lengo la kunogesha wimbo huo hasa kutokana na wenyeji wa michuano hiyo kuwa Brazil.
Zilipepea rangi za njano kwenye uwanja wa Arena de Sao Paulo na muda mchache baadaye ukachezwa mchezo wa ufunguzi kati ya wenyeji wa michuano  ambao walishinda kwa mabao 3-1 mbele ya  Croatia.
Shakira - Waka Waka (2010)
Shakira Isabel alikuja na waka waka, ulikuwa wimbo mahusisi kuwa ni muda wa Afrika, kibao hicho kilivuma sana. Kama inayofahamika uwezo wake wa kucheza ulikuwa kivutio kwenye uwanja wa Soccer City, Johannesburg nchi Afrika Kusini.
Mavuvuzela yalimsindika shakira kwenye uzinduzi huo ambao uliwakusanya Waafrika wote pamoja kwa kupata uwenyeji huo wa kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
Muda mchache baadaye ukafuata mchezo rasmi wa ufunguzi kati ya wenyeji, Bafana Bafana ambao walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mexico huku bao la kwanza la mashindano hayo likifungwa na Siphiwe Tshabalala.
Divo - The Time of our Lives (2006)
Il Divo ni kundi ambao lilikuwa linawajumuisha pamoja Urs Bühler (Switzerland), Carlos Marín (Spain), David Miller (USA), na Sébastien Izambard (France) wakali hao wa masauti waliumiza vichwa na kuja na hicho chuma chenye mpangilio mzuri wa sauti.
Sauti zao zilizokuwa zikipishana vyema kwenye kupanda na kushuka zilisika kwenye uwanja wa FIFA WM Stadion München, mjini  Munich kabla ya Ujerumani kuwatandika mabao 4-2 Costa Rica.
Sauti zao zilisikika zikiimba, Kulikuwa na ndoto, Muda mrefu uliopita, Ilipangwa kukua….Hilo limetuleta pamoja, ndoto waliyoizungumzia ilikuwa ni kuanza kwa michuano hiyo ambayo aliitwaa, Italia kwa kuifunga Ufaransa kwa penalti  5-3 baada ya sare ya bao 1-1 katika dakika 90.
Anastacia – Boom (2002)
Anastacia Lyn Newkirk alitumbuiza uwanja wa taifa wa Busan Asiad kwenye mji wa  Busan ambao upo Korea Kusini, Mmarekani huyo alitunga wimbo huo uliobeba ujumbe wa ugumu wa michuano hiyo.
Msanii huyo kwenye kibao chake hicho, alianza kuimba kwa kusema ni ngumu kujua nini utavuna katika mashindano hayo kutokana na ugumu wa michauno hiyo pengine ambayo huwa inafanyika kila baada ya miaka miwili.
Martin- The Cup of Life (1998)
Go, go, go! Ale, ale, ale! Wapenda soka wanaweza kusahau huu wimbo au hata wasiwe na uwezo wa kuuimba ila kwenye hicho kiipande unakuta wanaunga, Ricky Martin alibamba na kibao hicho alichotumbuiza kabla ya mchezo wa ufunguzi.
Utunzi wa Martin ulisema hilo ni kombe la maisha, wimbo huo ulijikita kwenye kuhamasisha wapenda soka na wadau mbalimbali kuelekea kwenye michuano hiyo ambayo ilikuwa ikifanyika kwa mara  ya 16.