Ndugu waliowahi kutamba kwenye Ligi Kuu England hawa hapa

Muktasari:

  • Hata hivyo, hao si ndugu wa kwanza kuwahi kucheza timu moja kwenye Ligi Kuu England baada ya kuwapo nyota wengine kibao kufanya hivyo.

MASTAA wa Ghana, Andre na Jordan Ayew wameandika historia mapema mwaka huu kwa kuwa ndugu wawili wengine kuwahi kuchezea timu moja ya Ligi Kuu England na kitu kizuri kucheza mechi pia ya ligi hiyo wakiwa wote uwanjani.

Hata hivyo, hao si ndugu wa kwanza kuwahi kucheza timu moja kwenye Ligi Kuu England baada ya kuwapo nyota wengine kibao kufanya hivyo.

Gary na Phil Neville

Timu: Man United

Mechi za ligi: 181

Hawa ni moja ya ndugu maarufu zaidi waliowahi kutamba kwenye Ligi Kuu England. Familia hiyo ya Neville ilifanya mambo yake kwenye kikosi cha Manchester United, ambako walicheza mechi kibao na kushinda mataji mengi tu, kabla ya mmoja kwenda Everton na mwingine kustaafu akiwa kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.

Gary alikuwa beki wa kulia, wakati mwenzake alikuwa kiraka, akicheza beki ya kushoto na wakali mwingine kiungo wa kati kulingana na matakwa ya kocha wa wakati huo, Sir Alex Ferguson.

Fabio na

Rafael da Silva

Timu: Man United

Mechi za ligi: 3

Ni ndugu wengine waliowahi kuitumikia Manchester United kwenye Ligi Kuu England. Lakini, wawili hao hawakufikia mafanikio makubwa kwenye ligi hiyo wakiwa pamoja, baada ya kucheza mechi tatu tu.

Tena katika mechi hizo tatu, wamecheza dakika 52 tu na walikuwa pamoja waliitumikia timu hiyo kati ya mwaka 2009 na 2012.

Fabio, alikuwa beki wa kushoto, wakati pacha wake alikuwa beki wa kulia. Kitu kibaya ni kwamba Rafael aliibukia vyema upande huo kwa sababu Gary Neville alikuwa hayupo, lakini kule upande wa kushoto kulikuwa na Patrice Evra bado anacheza. Fabio ilibidi tu aondoke, aende Queens Park Rangers.

Kolo na Yaya Toure

Timu: Man City

Mechi za ligi: 47

Kaka wawili wa familia moja waliowahi kukipiga kwenye Ligi Kuu England ni hawa, Yaya na Kolo Toure. Wawili hao kuna nyakati walikuwa wapinzani, lakini kuna nyakati nyingine walikwenda kucheza timu moja ya Manchester City.

Tofauti ya wawili hao ni kwamba Kolo alichezea timu nyingine akipiga Arsenal na Liverpool, wakati ndugu yake alidumu kwenye timu moja tu, Man City hadi mwishoni mwa msimu huu alipotangaza kuachia ngazi. Yaya angeweza kucheza pamoja na ndugu yake huko Arsenal, lakini akakosa kibali cha kufanya kazi na hivyo akatimkia Ukraine.

Andre na

Jordan Ayew

Timu: Swansea City

Mechi za ligi: 8

Wakiwa watoto wa gwiji wa mpira si jambo la kushangaza kuwaona watoto wake wakifanya vizuri pia kwenye mchezo huo ikiwamo kutamba kwenye Ligi Kuu England.

Baada ya kutamba Ufaransa, ndugu hao wawili, raia wa Ghana walitua kwenye Ligi Kuu England na kujikuta wakicheza pamoja kwenye kikosi cha Swansea City licha ya kwamba kuna nyakati kila mmoja alikuwa na timu yake, Andre akiitumia West Ham United na Jordan Aston Villa. Wawili hao walicheza pamoja kwenye kikosi cha Swansea kuanzia Januari. Baba yao ni Abedi Pele.

Shola na

Sammy Ameobi

Timu: Newcastle

Mechi za ligi: 4

Wakati Shola akiingia kwenye miaka yake ya mwisho ya mchezo wa soka, ndugu yake Sammy ndiyo kwanza alikuwa akiibukia. Wawili hao wametofautiana umri wa kiasi kikubwa sana, lakini jambo zuri ni kwamba waliwahi kucheza pamoja kwenye timu moja katika mechi ya Ligi Kuu England huko Newcastle United. Familia ya wakali hao wote ni washambuliaji na hakika wameonyesha kuwa na viwango bora kabisa katika ligi hiyo yenye umaarufu mkubwa duniani.

Wachezaji wengine

Kuonyesha Ligi Kuu England kulikuwa na ndugu wengi, baadhi yao ni Bradley na Shaun Wright-Phillips, waliocheza mechi 12 pamoja huko Man City, wakati Martin na Marcus Olsson walikuwa kwenye kikosi cha Blackburn Rovers na kucheza mechi 10, huku Gary na Steven Caldwell wao waliichezea Wigan Athletic mechi mbili walizokuwa pamoja. Rodney na Raymond Wallace wao waliitumikia Reeds United medhi sita, huku James na Adam Chambers wakiwa kwenye kikosi cha West Brom walicheza mechi moja tu na ndugu wengine walikuwa Stefan na Luke Moore huko Aston Villa waliocheza mechi moja na Alan na Stephen Quinn kwenye kikosi cha Sheffield United, ambao walicheza mechi moja. Christian na Jonathan Benteke (Crystal Palace, 2016/17), John Arne na Bjorn Helge Riise (Fulham, 2011/12) walitisha enzi zao.