Ndoa ya Alikiba gumzo kila kona Mombasa

Mombasa, Kenya. Haiwi haiwi imekuwa, asubuhi ya leo mapema harusi ya msanii Alikiba ilifanyika kwa shangwe jijini Mombasa.

Kiba aliandamana na nduguye Abdu Kiba walifika katika msikiti wa Ummul Kulthum wakiwa na rafiki yake wa karibu Alikiba Gavana Hassan Joho.

Baada ya aya chache za korani kusomwa muda ukawadia na Sheikh Mohammed Kagera akashika kiganja cha Alikiba kumuozesha mchumba wake Amina Khalef.

Baadaye AliKiba akatamka: “Mimi Ali Saleh nimekubali kumuoa Amina Khalef kwa mahari tuliosikizana na ikitokea sababu ya kuachana tuachane kwa wema.”

Tabasamu yake ya kawaida ikaja kinywani mwake baada ya kuitika mwito huo. Kiba alikuwa amevalia gauni linalitambulika kama Joho na kilemba na kushika upanga kama ilivyo desturi ya tamaduni ya Uswahilini.

Baada ya kutoka msikitini waalikwa walienda nyumbani kwa nduguye Joho, Abu Joho eneo la hapo Kizingo.

Baadaye mlo utakuwepo katika jumba la kifahari linalomilikiwa na Joho eneo la kaunti ya Kilifi.