Ndanda hii sio ile mjue

Muktasari:

Ndanda ikicheza soka maridadi mbele ya Wekundu wa Msimbazi, waliwabana watetezi hao na kutoka nao suluhu kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona na kuvuna pointi moja na ya kwanza kwake mbele ya Simba kwa misimu mitano mfululizo.

LICHA ya Kocha Patrick Ausems jana Jumamosi kuamua kuwachezesha kwa pamoja mastraika wake watatu wakali, Emmanuel Okwi, John Bocco na Meddie Kagere, aliishuhudia timu yake ya Simba ikibanwa na Ndanda mjini Mtwara.

Ndanda ikicheza soka maridadi mbele ya Wekundu wa Msimbazi, waliwabana watetezi hao na kutoka nao suluhu kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona na kuvuna pointi moja na ya kwanza kwake mbele ya Simba kwa misimu mitano mfululizo.

Simba kwa misimu minne ya nyuma ilikuwa ikijiokotea tu pointi kiulaini kwa wapinzani wao hao, lakini jana walikutana na sapraizi ya aina yake ambayo iliifanya Simba kufikisha alama saba baada ya kucheza mechi tatu.

Ndanda wao watakuwa na furaha baada ya kuvunja rekodi ambayo uliwekwa na Simba ya kucheza mechi nane dhidi ya timu hiyo kuchukua pointi katika mechi za nyumbani na ugenini.

Katika mechi nane za awali Simba ilivuna pointi zote 24, kabla ya jana Ndanda kuthibitisha kuwa, imebadilika na kukataa kuwa wateja wa kudumu wa Msimbazi na kuambulia suluhu hiyo iliyowafanya nyota wa timu hiyo kupewa Sh 2 milioni papo hapo kama ahsante yao kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa.

Kocha Aussems aliyemuacha msaidizi wake, Masoud Djuma jijini Dar es Salaam, aliamua kuchezesha washambuliaji hao na kumuanzisha Mohammed Ibrahim ili kusaka mabao mapema, lakini vijana wake walipata ugumu mbele ya mabeki wa kati wa Ndanda Malika Ndeule na Rajabu Rashid.

Mabeki hao na wengine walitibua mipango ya Simba na kufanya hadi mapumziko matokeo kuwa 0-0 licha ya kuwepo kwa kosa za hapa hapa na pale.

Katika mchezo huo ambao ulishuhudia Simba ikipata kona mbili tu na wenyeji Ndanda ikipata moja, Mbelgiji aliamua kuwatoa Okwi na Kagere kipindi cha pili kuwapisha James Kotei na Adam Salamba mabadiliko ambayo hayakubadili kitu.

Nahodha wa Simba, John Bocco alikiri pambano lilikuwa gumu na kwamba wanashukuru wamepata alama moja na sasa wanasahau kila kitu na kuangalia mechi zao zijazo zitakazochezwa Kanda ya Ziwa dhidi ya Mbao na Mwadui.

Katika mechi yao ya mwisho kwenye Uwanja huo, Ndanda ililazwa mabao 2-0 na Simba iliyokuwa chini ya Kocha Masoud na mabao yote yakifungwa na Bocco.

Katika viwanja vingine jana, Prisons ikiwa nyumbani ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na Ruvu Shooting, huku Mbao ikilala nyumbani bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania na kukwea kileleni ikiwa na pointi nane. KMC nayo imepigwa 1-0 na Singida United.

Mapema Lipuli ikiwa nyumbani mjini Iringa ililazimishwa suluhu na Mtibwa Sugar kama ilivyokuwa kwa Biashara United na Kagera Sugar mjini Musoma.