Mzigo wa Pre-Season Huu Hapa Unaambiwa

Muktasari:

  • Katika ratiba hiyo ya mechi za kujiandaa na msimu ujao, Liverpool itatesti mitambo yake kwa Manchester United na Manchester City katika kipindi hicho cha majira ya kiangazi wakati wa mechi hizo ambazo zitakuwa kwenye michuano ya International Champions Cup.

LONDON, ENGLAND

MAMBO ni moto unaambiwa. Ligi Kuu England ikiwa imebakiza mechi zisizozidi sita kwa kila timu, tayari ratiba nzima ya mechi za kujiandaa na msimu ujao zinazohusu vigogo wa Top Six imeshatoka.

Katika ratiba hiyo ya mechi za kujiandaa na msimu ujao, Liverpool itatesti mitambo yake kwa Manchester United na Manchester City katika kipindi hicho cha majira ya kiangazi wakati wa mechi hizo ambazo zitakuwa kwenye michuano ya International Champions Cup.

Inavyosomeka, Liverpool itacheza na Man City, ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu England msimu huu, Julai 25 huko New Jersey, Marekani kabla kukipiga na Man United siku tatu baadaye, Michigan.

Kabla ya hapo, Jurgen Klopp na kikosi chake hicho cha Liverpool atakuwa ametokea kumenyana na Borussia Dortmund, ambapo mechi hiyo itafanyika Julai 22 kwenye Uwanja wa Bank of America, North Carolina.

Guardiola atajiandaa na kampeni ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu England kwa kucheza na Dortmund, Julai 20 na atakipiga pia na Bayern Munich huko Miami.

Jose Mourinho na kikosi chake cha Man United na Mauricio Pochettino wa Tottenham Hotspur nao watakuwa na mechi huko Marekani.

Ukiweka kando Liverpool, Man United itacheza pia na AC Milan na Real Madrid, wakati Spurs itakipiga na AS Roma, Barcelona na AC Milan mjini San Diego, Pasadena na Minneapolis.

Arsenal itacheza kwenye michuano hiyo, lakini yenyewe itakuwa upande wa huko Singapore na Ulaya. Kikosi hicho cha Arsenal kinachonolewa na Kocha Arsene Wenger kimepangwa kucheza na Atletico Madrid, Julai 26 na Paris Saint-Germain Julai 28 kabla ya kwenda Stockholm kumenyana na wababe wenzao wa London, Chelsea Agosti 4.

Chelsea, ambayo itakwenda kutumia michuano hiyo kutafakari hali yake ya msimu huu, yenyewe itakipiga pia na Sevilla na Inter Milan, ambapo mechi hizo zitafanyika huko Poland na Sweden.

Hata hivyo, kwenye mechi hizo, vikosi hivyo vya Ligi Kuu England havitakuwa na mastaa wake wote kwa sababu wengi wao watakuwa wamekwenda kuzichezea timu zao za taifa kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia ambapo fainali yake itapigwa Julai 15, jambo ambalo wachezaji watakaokuwa kwenye fainali hizo watalazimika kupata mapumziko.