Mzee Majuto kufanyiwa upasuaji tena

Muktasari:

Mzee Majuto amelazwa katika hospitali ya Tumaini Jijini Dar es Salaam, alifanyiwa opereshini ya tezi dume Januari mwaka huu katika hospitali hiyohiyo.

Dar es Salaam. Muigizaji mkongwe Amri Athumani ‘Mzee Majuto’,  aliyelazwa leo katika hospitali ya Tumaini, anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa pili baada ya kidonda chake kushindwa kuziba.

Mzee Majuto amelazwa katika hospitali ya Tumaini Jijini Dar es Salaam, alifanyiwa opereshini ya tezi dume Januari mwaka huu katika hospitali hiyohiyo.

Mzee Majuto alisema pamoja na kuwa na kidonda, maumivu katika nyonga ndiyo yanamtesa zaidi.

Akizungumza na MCL Digital, leo Aprili, mke wake  Aisha  Yusufu, 23, alisema wamemfikisha mme wake hospitalini hapo baada ya hali yake kuwa mbaya na akiwa hawezi kutembea kutokana na maumivu anayoyapata.

“Yaani hapa tumekuja tumemshika na hata ukimwachia atembee inabidi atumie magongo kutokana na maumivu aliyonayo.

“Pia shida kubwa anayolalalmikia ni maumivu katika nyonga ambayo yanamfanya ashindwe kukaa wala kusimama na hata kula anakula akiwa amelala, naomba watanzania mumuombee mme wangu,”alisema mama huyo wa watoto wanne.

Aisha alisema operesheni hiyo ya pili itafanyika ili kujua ni nini tatizo la kidonda hicho kushindwa kupona mpaka sasa na tayari ameshachukuliwa vipimo wanachosubiri ni majibu na maamuzi ya madaktari.