Mwanza, Dodoma kushuhudia uhondo tamasha la pasaka

Dar es Salaam. Malkia wa Muziki wa injili nchini, Rose Muhando atazindua albamu yake mpya ya ‘Usivunjike Moyo’ katika Tamasha la Pasaka litakalofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Mkurugenzi wa Msama Promotins, Alex Msama amesema waimbaji wote watakaoshiriki tukio hilo linalosubiriwa kwa hamu, kwa sasa wapo katika mazoezi.

Alisema ya kwamba, awali tamasha hilo lilikuwa lifanyike katika mikoa miwili tu ya Mwanza hapo (Aprili Mosi) na Simiyu (Aprili 2), lakini sasa litafanyika pia mkoani Dodoma katika Uwanja wa Jamhuri Aprili 8.

“Tumeamua kuongeza kituo kingine cha tatu kwa ajili ya tamasha la Pasaka la mwaka huu, hivyo baada ya Mwanza na Simiyu, Aprili 8, uhondo utakuwa Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma,” alisema.

Waimbaji wengine katika tukio hilo ni Angel Benard, Paul Clement, Christina Shusho, Beatrice Mwaipaja, Bonny Mwaitege, Ephraem Sekereti kutoka Zambia, Jesca Honole na wakali wengine.

Viingilio vya tukio hilo ni kwamba, katika Uwanja wa CCM Kirumba; wakubwa watalipa Sh5,000 huku watoto wakilipa Sh2,000 na mkoani Simiyu; wakubwa watalipa Sh3,000 na watoto itakuwa Sh2,000.

Msama alisema mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba katika tamasha la Mwanza litakalofanyika Uwanja wa CCM Kirumba.

 “Mara zote baadhi ya waimbaji wamekuwa wakiimba live kwa kutumia vyombo jukwaani, hata safari hii itakuwa hivyo ili kuongeza mvuto zaidi kwa kila atakayefika uwanjani,” alisema Msama.