Mussa Mgosi apewa rungu Msimbazi

KOCHA wa kikosi cha Simba B, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amekabidhiwa kazi ya kujenga kikosi huku mwenyewe akitamba anaweza kuifumua timu yoyote kwa sasa.

Mgosi aliyewahi kutamba na Simba na Mtibwa Sugar, alianza kazi hiyo baada ya kuhitimu kozi ya ukocha na ameliambia Mwanaspoti: “Najisikia mwenye furaha kufanya kazi ninayoipenda, sioni changamoto yoyote. Nina malengo ya kuwa kocha bora nchini na duniani kwa jumla, ndiyo maana napambana kuhakikisha kazi yangu inakuwa nzuri, nataka kuwa kama Zidane au Pep Guardiola.

“Ni mwanzo lakini nina amini kikosi changu ninachokitengeneza kina uwezo mkubwa hata wa kucheza na timu za ligi kuu tukapata matokeo mazuri bila matatizo. Najiamini kwa sababu nimeanza nao mwenyewe tangu mwanzo kwa kuwafanyia majaribio na kupata wachezaji ninaowahitaji na kufanya nao kazi.”

ATAMBULISHA PROGRAM MPYA

Mgosi ambaye kikosi chake kinacheza mechi tofauti za kirafiki dhidi ya timu za Ligi Daraja la Kwanza na la pili, aliongeza: “Kwa sababu ya kuimarisha, nataka kupeleka maombi timu ya wakubwa, kila wanapocheza mechi ya ligi, wachezaji ambao hawajacheza, siku ya pili wacheze na timu B ili kuimaisha viwango vya timu zote.”