Mtanzania atua Nakumatt FC ya Kenya

Muktasari:

Kiungo huyo, ambaye amewahi kukipiga katika klabu ya Nakuru AllStars kabla ya kutua Chemelil Sugar, mwanzoni mwa mwaka jana, ameigura klabu hiyo inayokabiliwa na ukata mkubwa wa pesa.

Nairobi. Zikiwa zimesalia siku nane tu dirisha fupi la usajili la Kenya, lifungwe, klabu ya Nakumatt FC, inayoshiriki ligi kuu ya KPL, imemsajili Mtanzania Amani Kyatta, akitokea katika klabu ya Chemelil Sugar.

Kiungo huyo, ambaye amewahi kukipiga katika klabu ya Nakuru AllStars kabla ya kutua Chemelil Sugar, mwanzoni mwa mwaka jana, ameigura klabu hiyo inayokabiliwa na ukata mkubwa wa pesa.

Nakumatt FC, inayonolewa na Mmarekani Melis Medo, ilitangaza kuipata saini ya Kyatta lakini hakuna taarifa yoyote inaoelezea undani wa kandarasi aliyosaini na Nakumatt mpaka sasa. Kwa mujibu wa taarifa ya klabu hiyo, iliyotolewa kupitia ukurasa rasmi wa klabu kwenye mitandao ya kijamii, nyota huyo anakuwa wa tatu kusajiliwa.

"Tumefanya sajili tatu mpaka sasa na nyota wa tatu ni Amani Kyatta aliyetua akitokea Chemelil Sugar," ilisema taarifa hiyo. Kabla ya kutua katika ligi kuu ya Kenya, Kyatta, ambaye ni mzaliwa wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, amewahi kuichezea Morogoro United, timu ya taifa ya U20 na kikosi cha taifa stars.

Kyatta anaungana na Harun Nyakha na Joe Waithira aliyejiunga na Nakumatt wakitokea Wazito FC. Wakati huo huo, Nakumatt, inayoshika nafasi ya 12 kwenye jedwali la KPL, inamvizia beki wa Chemelil Sugar, Yusuf Juma.