Mjengo wa Samatta ni wa mastaa ulaya aisee

NI miaka miwili sasa tangu mshambuliajia wa Kitanzania, Mbwana Samatta anayekipiga KRC Genk ya Ubelgiji ajiunge na timu hiyo akitokea TP Mazembe ya DR Congo. Hivi sasa nahodha huyo wa Taifa Stars ameanza kupata ofa mbalimbali kutoka timu kubwa barani Ulaya ikiwemo CSKA Moscow ya Russia, Lerante ya Hispania, Maitiz na Hertha Berlin zote za Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga.

Hata hivyo, bado straika huyo hajaweka wazi wapi anaweza kwenda kucheza baada ya kuondoka Genk kwani, timu zote zimeonyesha nia huku Lerante ikitanguliza mguu mmoja mbele kwa kuweka mezani dau la Sh 10.6 bilioni.

Ubora wa Samatta unaongezeka kadiri siku zinavyosonga, hiyo yote ni kutokana na malengo pamoja na ndoto zake za kutaka kucheza Ulaya. Vitu vinavyomsaidia ni nidhamu, kujituma, kujiamini na kujitambua kile anachokifanya.

Sasa achana na mambo yake ya uwanjani pamoja na mafanikio akiwa ndani ya uwanja, Samatta amekuwa na uelewa mpana nje ya uwanja kwa kutambua kuna maisha baada ya kustaafu soka, hivyo ni lazima awekeze katika biashara na ardhi.

Samatta anamiliki ardhi katika maeneo mbalimbali nchini na amejenga zaidi ya nyumba tano nyingi zikiwa Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam ambako hasa ndiko nyumbani kwao. Baba yake mzazi, Ally Samatta Pazi anaishi Mbagala.

Samatta akiwa na TP Mazembe alijenga ghorofa maeneo ya Kibada wilayani Kigamboni. Ni ghorofa ambalo lilimalizika kabisa kwa maana mtu angeweza kuanza kuishi ndani yake.

Lakini baadaye Samatta hakufurahishwa na kile kilichoonekana baada ya kukamilika kwa ujenzi huo, alisema halikuwa kwenye hadhi na ubora anaoutaka na kuamuru livunjwe lote fasta.

Baada ya kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora kwa Wachezaji wanaocheza Ndani ya Afrika mwaka 2016 akiwa TP Mazembe na wakati huo mkataba wake ulikuwa ukingoni na michakato wa kwenda Ulaya ilikuwa imeanza, alilivunja ghorofa hilo.

Ghorofa hilo lilidaiwa kutumia Sh 500 milioni pamoja na kujengwa kwa kiwango cha chini na ndipo Samatta, alipopatwa na uchungu wa kupoteza pesa kwa kitu ambacho hakikuwa kwenye ubora.

Samatta alitafakari kabla ya kutoa uamuzi huo mgumu wa na kuanza upya, hakujali gharama zilizotumika awali.

Mwanaspoti lilitembelea wakati ghorofa hilo likivunjwa, ujenzi mpya ulipoanza na sasa ghorofa hilo lilipofikia.

MJENGO WENYEWE

Nyumba hiyo ni ya ghorofa moja, kwa maana juu na chini. Chini ina vyumba viwili vya kulala kimoja ni ‘master bedroom’, jiko, sebule, chumba kwa ajili ya chakula, stoo, chumba maalumu kwa ajili ya mambo ya umeme, chumba cha kufulia nguo, chumba cha ibada, choo cha jumuiya.

Huko ghorofani utakutana na vyumba viwili vya kulala ambavyo vyote ni ‘master bedroom’ ni vyumba ambavyo ni vya kipekee kutokana na jinsi vilivyotengenezwa vyumba vya chini, chumba kimoja kimechorwa michoro kama katuni ambacho kinaonyesha ndicho cha watoto.

Kuna chumba ambacho kimeandaliwa kwa ajili ya kupumzika, ambapo pia utapata burudani ya sinema na mzuka wote wa soka.

Bado kuna chumba kingine kwa ajili ya mikutano na shughuli nyingine, ambapo pia kuna sehemu maalumu kwa ajili ya kupata upepo. Eneo hilo kwa chini Samatta atakuwa akipata mandhari mwanana ya bustani, bwawa la kuogelea, uwanja wa michezo.

Kwa jumla ni kwa mtu mwenye haraka ya kuhamia anaweza kuhamia wakati mambo mengine madogo madogo yakiendelea kumaliziwa.

GHARAMA

Wakati ghorofa la mara ya kwanza lililobomolewa lilijengwa kwa Sh 500 milioni lakini ghorofa hili la kisasa linadaiwa kutumia karibu Sh 1 bilioni hadi hapo lilipofikia ingawa bado halijamalizika vitu vidogo ikiwemo kuwekwa urembo.

Kila kitu ambacho kinatakiwa kuwemo ndani ya nyumba kimenunuliwa tayari ikiwemo samani za ndani na vikorombwezo kibao Mzee Samatta, ambaye alikuwa ndiye mwenyeji wa Mwanaspoti alisema pesa nyingi zimetumika kwenye mjengo huo.

“Hapa bado pesa itaendelea kutumika, kwani bado malengo yake hajakamilika ili aweze kuhamia. Ingawa kwa asilimia kubwa amekamilisha.

“Mwanangu amewaza jambo jema ambalo linastahili kuigwa na amenifurahisha mzazi wake kwani, peke yake ndiye amefuata akili zangu kwa asilimia kubwa, Mungu amfungulie zaidi milango yake.”

AJENGA MSIKITI

Kama hufahamu Samatta ameanza kurudisha shukrani kwa wananchi wanaompa sapoti na kumshukuru Mungu. Kila kitu anaamini katika Mungu kuwa ndiye pekee anayempa uwezo wa kupambana na kuwafanya, hata mashabiki wampende ni Mungu, basi ameaanza ujenzi wa Msikiti.

Achana na Msikiti uliopo ndani ya mjengo wake huo, ambao atautumia yeye na familia yake itakayoishi hapo pamoja na marafiki zake, Samatta pia ameanza ujenzi wa Msikiti katika Kijiji cha Kidubwa ambacho kipo Kitongoji cha Picha ya Ndege huko Vikindu wilayani Mkuranga.

Fundi anayejenga Msikiti huo, Yusuph Ahmad ambaye pia ndiye anayejenga ghorofa hilo tangu awali amefafanua: “Mpango wetu huu Msikiti tunataka umalizike kwa kipindi cha mwezi mmoja labda mambo yaingiliane tu, ila kila kitu kinakwenda sawa.

“Ile nyumba kule imechelewa kuimalizika kwa sababu kuna mambo hayakwenda kama tulivyokuwa tumepanga ndiyo maana tumechukua zaidi ya miaka miwili, lakini hatua iliyobaki ni ndogo kwa upande wa nyumba.

“Kwanza tulijenga ukuta ndipo ikafuata nyumba, bado kule chini ambako ana mpango wa kuweka vitu vingine kama uwanja, sehemu ya bwawa la kuogelea,” alisema Yusuph.

KITUO CHA MICHEZO

Katika kuendelea kurudisha shukrani kwa wadau wa michezo na wananchi kwa jumla, Samatta ana mpango wa kujenga kituo cha michezo katika Kijiji ya Mwanzega kilichopo Mkuranga, eneo hilo la ekari tano alipewa na serikali.

“Ana eneo kubwa ambalo atajenga kituo cha michezo, hospitali, uwanja wa mpira, sehemu nyingine itakayobaki ataamua ajenge nini, ni zawadi aliyopewa na serikali, naamini akikamilisha haya yote ndipo atakapoanza huko kwani, ana hamu ya kutekeleza kila kitu alichokipanga,” alisema Mzee Samatta.

Mbali na eneo hilo huko Mkuranga, pia Samatta ana eneo lingine alilopewa na serikali ambalo lipo Kibada, lakini bado hajapanga atajenga nini ama atalifanyia kazi gani.

KITABU CHA SAMATTA

Mzee Samatta tayari amekamilisha utunzi wa kitabu kinachomuhusu mwanaye huyo kinachoitwa ‘Huyu ndiye Mbwana Samatta’ ambacho kimeanza kuuzwa kwa Sh 5,000.

“Hiki kitabu kina historia nzima ya Samatta katika soka, nimekiandaa mwenyewe, niliona niandike kitabu kama kumbukumbu na kuwafahamisha watu wamfahamu zaidi Samatta alikotoka kisoka.

“Lakini, kuna kitabu kingine kinakuja ambacho kinanihusu mimi. Naandika vitabu ili wadau wa soka wajue chimbuko letu katika michezo hasa soka,” alisema Mzee Samatta.

AGOMA KUKAA KWA SAMATTA

Imeelezwa Samatta alikuwa na mpango wa kumzawadia baba yake hilo ghorofa, lakini Mzee Samatta amegoma kabisa.

“Kama ningekubali, muda huu ningekuwa nimehamia hapa. Alitaka nihamie hata sasa lakini binafsi nataka kuishi sehemu nyingine, hivyo amepanga kunijengea.

“Nahitaji sehemu ambayo nitalima mazao na sio hapa hakuna eneo hilo, kuna sehemu ndogo ambayo anataka awe analimalima mboga, kwangu hapanifai.

“Pia, kumetulia sana, haya ni maisha ya peke yako, namshukuru sana ila nitakwenda kuishi huko kwingine atakakonijengea, nitalima kila kitu na kujiachia,” alisema Mzee Samatta.