Mbunge Chumi amkosoa rais wa TFF, Malinzi na kutaka damu mpya kwenye uongozi wa shirikisho hilo

Muktasari:

Chumi alisema kiongozi anapimwa kwa mafanikio katika kipindi chake cha uongozi, lakini Malinzi ameshindwa licha ya kujengewa misingi na mtangulizi wake Leodegar Tenga

Dar es Salaam. Mbunge wa Jimbo Mafinga Mjini, Cosatu Chumi amesema rais wa sasa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameshindwa kusaidia maendeleo ya soka nchini.

Chumi alisema kiongozi anapimwa kwa mafanikio katika kipindi chake cha uongozi, lakini Malinzi ameshindwa licha ya kujengewa misingi na mtangulizi wake Leodegar Tenga.

“Tukifanya tathimini utaona kabisa hakuna mafanikio tuliyotarajia kama alivyokuwa amejenga msingi imara Tenga (Leodgar), hawa walikuta tayari mifumo imejengwa, badala yake soka letu linazidi kudidimia,” alisema Chumi.

Aliongeza kuwa kwa Tanzania imeporomoka kwenye viwango vya Fifa, ushindani wa Tanzania kwenye michuano ya Afrika umekuwa chini tofauti na miaka ya nyuma.

“Hawa waliochukua fomu sioni namna wanayoweza kutuvusha, tunahitaji damu mpya na fikra mpya za kutufikisha tunakotaka,”alisema mbunge huyo aliyeingia bungeni baada ya uchaguzi wa 2015.