Mbappe aweka rekodi, France ikiitungua Peru 1-0

Moscow, Russia. Ikiwa ni bao lake la kwanza katika michuano ya Kombe la Dunia tangu aanze kusakata kabumbu, Kylian Mbappe, ameweka rekodi yankuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuifungia timu ya taifa ya Ufaransa katika michuano hii ya Kombe la Dunia.
Straika huyo wa  Paris Saint-Germain, amevunjilia mbali rekodi ya muda mrefu iliyowekwa na nyota wa zamani wa France, David Trezeguet, iliyodumu kwa miaka 20. Trezeguet alifunga bao lake katika michuano ya Kombe la Dunia ya mwaka 1998, yaliyofanyika nchini Ufaransa, akiwa na miaka 20.
Mbappe mwenye umri wa miaka 19 na siku 183, alikwamisha mpira wavuni, akiunganisha shuti la Olivier Giroud. Kufuatia ushindi huo, wa kundi C dhidi ya Peru, Ufaransa sasa wanaongoza kundi lao na wamefanikiwa kutinga hatua inayofuata ya 16 bora.
Katika mchezo unaofuata, ambao ni mchezo wa mwisho wa makundi, Ufaransa watakutana na Denmark ambayo nayo imeshavuka hadi hatua inayofuata. Kwa upande wao, Peru watamaliza ratiba dhidi ya Australia ambayo nayo iko mbioni kuaga mashindano ya mwaka huu.