Mbappe, Neymar Madrid inawahusu

Muktasari:

Kwenye dirisha lililopita, Perez alihusishwa na mpango wa kutaka kufanya usajili wa kushtua dunia kwa kuwanasa mastaa wa Paris Saint-Germain, Kylian Mbappe na Neymar

MADRID, HISPANIA.Real Madrid imeripotiwa kuwa na Pauni 330 milioni za kutumia na rais wa klabu hiyo, Florentino Perez amepanga kushusha masupastaa tupu kwenye kikosi chake katika dirisha lijalo la usajili.
Hizo ni taarifa za kipesa zinazoripotiwa kutoka Hispania. Ripoti zinadai kwamba Real Madrid wamekusanya pesa za maana na hapa mpango wao wa kwanza ni kuhakikisha wanakamilisha ndoto zao za kunasa wachezaji wenye majina na wenye umahiri kufanya maisha ya Bernabeu kuwa matamu.
Kwenye dirisha lililopita, Perez alihusishwa na mpango wa kutaka kufanya usajili wa kushtua dunia kwa kuwanasa mastaa wa Paris Saint-Germain, Kylian Mbappe na Neymar. Lakini, wababe hao, Los Blancos walihusishwa pia na Eden Hazard kwamba angejiunga na timu yao baada ya Cristiano Ronaldo kuhamia Juventus. Walichofanya kwanza ni kumnasa kipa Thibaut Courtois na kwamba dirisha likifunguliwa tena, hizo Pauni 330 milioni ndio zitaanza kufanya kazi.
Kinachoelezwa ni kwamba hakuna kitakachozuia kwenye usajili unaokuja kwamba mmoja kati ya mastaa hao, Neymar, Mbappe na Hazard asitue Real Madrid, huku kukiwa na ripoti wanaweza kunaswa mastaa wawili kwa mpigo. Madrid imeripotiwa inacheki kwa umakini vyanzo vyake vya kipesa kuhakikisha inakuwa na nguvu wakati madirisha ya usajili yatakapofunguliwa mwakani.