Mayweather, Pacquiao kukiwasha upya Desemba

Muktasari:

Mara ya kwanza walipokutana kati ya Mmarekani huyo na Mfilipino Pacquiao (39) pambano lao lilitikisa ulimwengu wa ngumi na kupewa jina la 'The Fight of the Century'.

Tokyo, Japan. Bondia Floyd Mayweather amesema atarejea ulingoni kwa lengo mmoja tu la kupambana na Manny Pacquiao mwishoni mwa mwaka huu.

Wawili hao walikutana mara mwisho Las Vegas mwezi Mei 2015, na Mayweather kuibuka mshindi kwa pointi.

Mayweather alituma video katika mitandao ya kijamii akisema: "Narudi kupigana na Manny Pacquiao mwaka huu. Dau lingine nono linakuja akaeni tayari."

Bondia huyo mwenye miaka 41, hajashiriki pambano lolote tangu alipomshinda nyota wa UFC, Conor McGregor mwezi Agosti 2017.

Alitangaza kustaafu ngumi baada ya pambano lake la raundi 10 simamishwa na kutangazwa mshindi dhidi ya McGregor, na kuweka rekodi ya kushinda mapambano 50-0.

Mara ya kwanza walipokutana kati ya Mmarekani huyo na Mfilipino Pacquiao (39) pambano lao lilitikisa ulimwengu wa ngumi na kupewa jina la 'The Fight of the Century'.

Naye bondia Muingereza Amir Khan aliweka wazi kuwa lengo lake na kupigana na Pacquiao baada ya ushindi wake dhidi ya Samuel Vargas mwanzoni mwa mwezi huu.