Mastaa Simba, Yanga wavutwa Arusha

Muktasari:

Mchezo huo, uliopigwa Uwanja wa sheikh Amri Abeid jijini

Arusha ukiwa na lengo la kupunguza ajali na kukuza ushirikiano baina ya madereva hao wanapokuwa barabarani.

Arusha. Wachezaji Ibrahim Ajib wa Yanga pamoja na Jonas Mkude na Shiza Kichuya wa Simba wameshuhudia kipigo cha madereva wa Bodaboda kutoka kwa wale wa daladala ambao walishinda kwa penalti 3-2.

Mchezo huo, uliopigwa Uwanja wa sheikh Amri Abeid jijini Arusha ukiwa na lengo la kupunguza ajali na kukuza ushirikiano baina ya madereva hao wanapokuwa barabarani.

Wachezaji hao watatu walikuwa wamekaa katika viti maalumu sehemu ya wageni rasmi kutokana na mwaliko wao na kushuhudia mtanange huo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Daladala ndiyo walitangulia kufunga bao dakika ya 25 kupitia kwa mchezaji wake, Juma Hassan. Kipindi cha pili Bodaboda waligomea ushindi huo na kusawazisha dakika ya 73 kupitia kwa  Abdul

Mzambia na kufanya dakika 90 za mchezo kuisha kwa sare ya 1-1 na mwamuzi kuamua mikwaju hiyo ya penalti ipigwe.

Kutokana na ushindi huo, Daladala imebeba kombe na kitita cha shilingi laki sita wakati boda boda wakipewa shiling laki nne tu.

Akizungumzia mashindano hayo, mgeni rasmi ambaye ni Katibu Tawala Wilaya ya Arusha, David Mwakiposa aliwataka madereva hao kuhakikisha wanatumia barabara wakijali wengine ili kupunguza

ajali.

Kwa upande wake mratibu Wa bonanza hilo, Ashura Mohamed alisema  kuwa wameamua kushirikisha timu hizo baada ya kuona Wingi Wa ajali barabani lakini pia kukuza ushirikiano.